TIBAIJUKA AMTAKA RAIS MAGUFULI ATUMIE HURUMA SAKATA LA WATUMISHI WALIOFUKUZWA KWA VYETI FEKI


Mbunge wa Muleba Kusini (CCM) Profesa Anna Tibaijuka amemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika kuangalia kitengo cha utawala bora kwani bado kuna shida.

Profesa Tibaijuka ametoa kauli hiyo jana Ijumaa Aprili 12, 2019 ambapo alisema kuna watu wanaumizwa kwa kisingizio cha uchunguzi haujakamilika . Sambamba na hilo pia alitaka waliofukuzwa kazi kwa kukosa vyeti vya kidato cha nne wahurumiwe.

Mbunge huyo amesema utawala bora ni pamoja na sheria na haki lakini katika eneo hilo kumekuwa na shida.

"Mimi napenda hoja, napenda majadiliano lakini napenda upinzani bora kwa hiyo hapa nazungumza kwa nia njema tu wala si kingine," amesema Tibaijuka.

Amesema suala la utawala bora ni pana na linatakiwa kuangaliwa kwa mapana yake huku akimtaja Waziri George Mkuchika na naibu wake, Mary Mwanjelwa kwamba ni wakati wa kusimama imara kuangalia jambo hilo.

Huku akishangiliwa na wabunge wa pande zote wa upinzani na CCM waziri huyo wa zamani amesema suala la utawala bora linagusa hata makandarasi wa ndani ambao hawalipwi madai yao jambo linalopelekea hofu ya kubaki wakandarasi wa China pekee.

Amelalamikia watumishi wanaofanya ukaguzi shule binafsi kwamba wamekuwa wakibambikiza madai ambayo hayana msingi wakitaka rushwa.

Katika hatua nyingine mbunge huyo amemwomba Rais John Magufuli kurejea huruma yake kwa watumishi waliofukuzwa kazi kwa kukosa sifa ya kidato cha nne kwamba waangaliwe.

Amesema kuna watu walikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi akitolea mfano wa Mbunge wa Mtera (CCM) Livingston Lusinde kwamba licha ya elimu yake ya darasa la saba lakini uwezo wake ni zaidi ya mtu mwenye shahada mbili.

Amezungumzia suala la vyeti kwamba suala la kutunza vyeti si jukumu la mtu bali Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) na vyombo vingine ndiyo watunze ili mtu akipoteza cheti mara moja akapate huko.

Profesa Tibaijuka ametolea mfano kuwa wapo maprofesa 10 hadi sasa wanahangaika baada ya kusimamishwa kwa kukosa vyeti vya kidato cha nne.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527