MSANII NIPSEY HUSSLE AUAWA KWA KUPIGWA RISASI


Rapper Nipsey Hussle wa nchini Marekani ameuawa kwa kupigwa risasi alfajiri ya leo, baada ya kuvamiwa na watu ambao mpaka sasa bado hawajajulikana.

Taarifa kutoka Los Angeles nchini Marekani zinasema kwamba tukio hilo limetokea nje ya duka lake la nguo, ambapo walikuja watu wakiwa kwenye gari na kuanza kummiminia risasi kadhaa zilizochukua uhai wake wakati akikimbizwa hospitali.

Kwenye tukio hilo watu wengine wawili wamejeruhiwa, kutokana na risasi zilizokuwa zikipigwa bila mpangilio.

Nipsey Hussle ambaye jina lake halisi ni Ermias Davidson Asghedom alikuwa na miaka 33, na alikulia Kusini mwa Los Angeles akiwa ni mwanachama wa kundi la vijana wa mtaani (Street gang) la Rollin 60s.

Muda mfupi uliopita rapper huyo aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa twiiter uliosema kwamba “kuwa na maadui wenye nguvu ni baraka”, jambo ambalo limehusishwa kuwa huenda alijua nini kinakuja kutokea kwake.

Nipsey ameacha mke na watoto wawili wa kike, huku akiwa na album moja iliyokuwa imetajwa kwenye tuzo za Grammy mwaka huu, kama album bora ya rap.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post