Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile ametoa sababu za kwanini hospitali ya wagonjwa wa akili ya Mirembe ilijengwa jijini Dodoma.
Dkt. Ndugulile ametoa sababu hizo wakati akijibu swali la Spika wa Bunge, Job Ndugai ambalo lilihoji kuwa, "wiki hii kumekuwa na ujumbe ukisambaa ukidai kwanini miradi mikubwa mingi iliwekwa mikoa mingine na Dodoma ikajengwa hospitali ya watu wenye ugonjwa wa akili? Unaweza ukatusaidia ufafanuzi kidogo", aliuliza Spika.
Katika majibu yake ya ufafanuzi kwa Spika, Ndugulile amesema kuwa hospitali hiyo ilijengwa pale kutokana na Gereza la Isanga ambalo lilikuwa likipokea watuhumiwa wa kesi za mauaji hivyo ilitakiwa wapimwe afya ya akili kabla ya kuhukumiwa.
"Sio kwamba wagonjwa wa akili wengi wako Dodoma la hasha!. Bali ni kutokana na uwepo wa gereza kubwa la Isanga na wengi wao pale walikuwa wakihukumiwa kwa makosa makubwa makubwa ya mauaji hivyo tulikuwa tunahakikisha kwanza wanapimwa afya zao za akili", amesema Dkt. Ndugulile.
Wiki hii kumekuwa na ujumbe ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambao ulikuwa ukisomeka; "Mwl. Nyerere acheni aitwe Baba wa Taifa, alikuwa anaona mbali sana kiwanda cha Katani alikijenga Tanga sababu Mkonge unastawi vizuri huko, akajenga Mwatex - Kiwanda cha Nguo huko Mwanza ambapo pamba inastawi vyema; na cha Kahawa kipo Moshi - sasa sijui kwa nini aliamua kujenga hospitali ya Milembe huko Dodoma".