JACQUELINE : SIJAFUATA PESA KWA MENGI BALI MAPENZI YA DHATI

Jacqueline Ntuyabaliwe ambaye ni mke wa mfanyabiashara maarufu Tanzania, Reginald Mengi, amesema kwa Mengi hajafuata fedha bali mapenzi ya dhati.

Ameyasema hayo leo Ijumaa, Aprili, 5, 2019 alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha XXL kinachorushwa na kituo cha Clouds kuelekea siku ya malkia wa nguvu ambapo pamoja na mambo mengine watangazaji walimtaka kutolea ufafanuzi kuhusu maneno ya watu kwamba kafuata fedha kwa Mengi.

Jacqueline amesema katika mapenzi mtu hapaswi kumjaji mtu kwa kumuangalia muonekano aliokuwa nao au fedha badala yake aangalie kama ana mapenzi ya kweli ili asije kujutia baadaye kwa nini aliingia kwenye mahusiano.

Akitolea mfano yeye, amesema amekuwa katika mahusiano na Mengi kabla ya kuingia kwenye ndoa kwa miaka mitatu, na hakuna ukweli wowote kwamba alifuata fedha kwake bali mapenzi ya kweli.

“Tunachosema vijana tunapoingia kwenye mapenzi ni kumjaji mtu kutokana na hadhi yake na muonekano wake, lakini wanapaswa kukumbuka fedha mtu anazokuwa nazo leo kesho huenda asiwe nazo,”amesema Jacqueline ambaye pia ni mjasiriamali.

Akimzungumzia Mengi ni mtu wa gani, amesema ni mpole na mwenye kujua mambo mengi na kuongeza kuwa licha ya kuwa mume wake ni rafiki na amekuwa mshauri mkubwa sana kwake tangu walipoanza mahusiano hadi kufikia hatua ya kuoana.

Wakati kuhusu suala la kuongeza watoto amesema hana mpango huo kwani katika kuomba kwake dua ilikuwa kupata watoto mapacha na anashukuru Mungu amemjalia kwa kumpatia watoto hao huku suala la kuzaa akisema amewaachia wengine.

Na Nasra Abdallah, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post