MAKAMU WA RAIS AWAJIBU WANAOHOJI ULINZI WA RAIS MAGUFULI


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewashangaa wanasiasa wanaohoji ulinzi wa Rais John Magufuli, badala ya kuhoji maendeleo yanayofanywa na serikali.



Samia amesema kwa kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli wasiofurahia wanaishia kuzungumza vitu visivyo na msingi huku akidai kwamba watu hao wamefilisika.

Makamu wa Rais ameyasema hayo jana Jumamosi Aprili 13, 2019 wakati wa hafla ya uzinduzi wa mji wa kiserikali uliopo Ihumwe mkoani Dodoma unaofanywa na Rais Magufuli. 



“Nilisikiliza dondoo za magazeti na kusikia mtu anahoji kuhusu ulinzi wa rais, nikajiuliza anahoji ulinzi ili iweje kwa nini asitumie muda huo kuhoji maendeleo yanayoendelea.

“Hii inaashiria kwamba jamaa zetu wameishiwa, wamefilisika na mawazo na nini wazungumze ndani ya nchi yetu, kwa sababu hawawezi kuzungumzia maendeleo haya watakuwa wanajitia kisu cha tumbo kwa hiyo sasa wanajiweka katika kuhoji vitu ambavyo havihitaji kuhojiwa, ila Watanzania tuko na wewe,” alisema.

Samia ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja imepita tangu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe juzi jioni akichangia mjadala wa bajeti ya ofisi ya Rais, Tamisemi na Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhoji ulinzi wa rais kuwa mkubwa.

Mbowe wakati akichangia elieleza kuwa amekutana na msafara wa Rais, lakini ameogopa kwa alichoeleza kuwa anasindikizwa na magari zaidi ya 80.

Akichangia suala hilo, Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM), amesema suala la ulinzi kwa Rais John Magufuli linahitajika liwe kubwa zaidi kutokana na mambo makubwa anayofanya ya kunyoosha nchi.

 Kingu alisema ;“Suala la ulinzi na usalama kwa Rais lazima liwe kubwa..nashauri ulinzi wa Raia uongezwe maradufu maana hatuwezi kuacha kutokana na mambo makubwa anayofanya hivyo usalama wake haupo sawa.” 

Kingu alifafanua kuwa kwenye suala la utawala bora hakuna mahali palipoandikwa kuwa chama fulani kifanye vurugu au kundi la watu fulani.

“Jimbo ninalotoka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) wameletewa kiasi cha shilingi bilioni 1.3, tuna madaraja na vituo vya afya hayo ni mambo ya utawala bora tunayohitaji,” alieleza.

Alifafanua kuwa hata kwenye Jimbo la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), serikali imepeleka maji katika vijiji vingi na watu wanafaidika na huduma hiyo licha ya kuwa hayupo.

“CCM chini ya Rais John Magufuli inafanya kazi kubwa na 2020 anachukua kura zaidi ya asilimia 95,” alisema.

Wakati Kingu akizungumza Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) aliomba utaratibu kwa mujibu wa Kanuni ya Kudumu ya Bunge namba 64 ambapo aliruhusiwa kuzungumza.

“Mheshimiwa Mwenyekiti tupo hapa kudhibiti matumizi ya fedha anachozungumzia Mbunge Kingu inaonesha kama Bunge tumepewa fadhila na serikali wakati tumekuja kusimamia kodi za wananchi,” alisema Msigwa 

Baada ya Msigwa kumaliza kuzungumza Mwenyekiti wa kikao hicho, Andrew Chenge alimtania Msigwa kwamba alikuwa na nia ya kuchangia tu.

“Lakini Kingu anatukumbusha sisi kama wabunge yanayofanywa na serikali kupitia bajeti bila kujali unatoka chama gani au ni mbunge gani maana serikali inasukuma maendeleo na ndio hoja yake,” alisema Chenge.

Aliongeza kuwa, “Tujenge hoja maana muda ni mdogo nawaombeni tutambue kuwa tunajenga nyumba moja hivyo Mbunge Kingu endelea kuchangia."


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527