MAANDALIZI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA YAANZA

Na.Alex Sonna/ Fullshangwe

Wakati  uchaguzi wa serikali za mitaa 2019, ukitarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) leo imekutana na wadau wa vyama vya siasa kwa ajili ya kupitia rasimu za kanuni za uchaguzi huo.

Hayo yamesemwa leo jijini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo wakati wa kufungua kikao cha kupitia rasimu ambapo ametaja  rasimu tatu ambazo wadau hao watazijadili kuwa ni pamoja na Rasimu ya kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya za mwaka 2019.

Waziri Jafo ametaja rasimu zingine kuwa ni ya Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za mwaka 2019 na Rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji midogo za mwaka 2019.

Aidha Jafo amewaomba wadau hao kutoa maoni na mapendekezo yatakayokuza demokrasia na utawala bora huku akiahidi kuwa serikali itazingatia maoni yao ili kanuni hizo ziweze kuleta tija na ufanisi kwenye uchaguzi.

Hata hivyo Jafo amesema utii wa Sheria za Nchi, Kanuni na Taratibu za Uchaguzi ndio msingi wa uchaguzi ulio wa haki na wenye kuzingatia ushiriki wa makundi yote ya jamii.

“Vyama vya siasa vinaowajibu wa kuwaelimisha na kuwaelekeza wagombea, wafuasi na wanachama wao kuzingatia matakwa ya Sheria za Nchi na kanuni hizi za uchaguzi wa serikali za mitaa,”amesema Jafo

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa John Shibuda  ametoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe ameshukuru kwa fursa hiyo waliyoipata na kuwataka wajumbe kuvumiliana na kutumia vizuri nafasi waliyoipata kwa maslahi mapana ya wananchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527