KANYASU AWATAKA ASKARI MISITU KUREJESHA UOTO WA ASILI

Na Tulizo Kilaga, TFS

Mlele. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Costantine Kanyasu amewataka askari wa misitu waliohitimu mafunzo ya kijeshi kuhakikisha wanarejesha katika uoto wake wa asili maeneo yote ya misitu ambayo yameharibiwa.

Mhe. Kanyasu, aliyasema hayo jana alipokuwa akifunga mafunzo ya kijeshi kwa askari 140 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kambi ya mafunzo ya kijeshi Mlele mkoani Katavi.

“Leo mmehitimu na tumewaapisha, mmekuwa askari kweli wa TFS lakini tambueni kuwa kazi za kiuchumi zinapelekea uharibifu mkubwa sana wa mazingira, na hatuwezi kusema zisiendelee, zinatakiwa kuendelea katika namna ambayo haitaifanya nchi yetu kuwa jangwa.

“Kuhitimu kwenu hakumaanisha mnakwenda kuzuia maendeleo, kunamaanisha mnakwenda kushirikiana na wanaotaka maendeleo kwa kufanya kazi wakifikiria maendeleo endelevu,” alisema.

Mhe. Kanyasu alisema hivi sasa nchi inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya tabia nchi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti, ukame, mvua nyingi na mafuriko ambapo vyote hivyo husababishwa na matumizi mabaya ya kazi za kiuchumi.

Alisema ni matarajio ya Serikali kuwa baada ya askari hao kuhitimu pamoja na kazi yao ya msingi ya ulizi watafanya kazi ya kuhakikisha wanarejesha uoto wa asili uliopotea.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo katika hotuba yake alisema Taifa limekuwa likikumbwa na changamoto mbalimbali za kiuhifadhi ikiwemo shughuli za kibinadamu pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa watumishi na mambo hayo yote yanasababisha mafunzo hayo kuwa muhimu katika uhifadhi wa mapori na misitu ya hifadhi nchini.

Prof. Silayo alisema pamoja na mafunzo hayo yanayofanyika, TFS inaimarisha vikosi vyake vya kufuatilia taarifa ambapo ina kitengo cha intelijensia ambacho wanakiimarisha ili kiweze kutoa taarifa sahihi kwa askari wa misitu na kuchukua hatua bila kupoteza wakati.

Zoezi hilo limehudhuriwa na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira pamoja na wananchi.

Wizara ya Maliasili na Utalii imebadili mfumo wake wa usimamizi wa maliasili toka ule wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi (Paramilitary). TFS imekuwa mstari wa mbele kwenda na mabadiliko hayo kwa kuanza kutekeleza mafunzo ya watumishi katika ngazi mbalimbali wakati ikisubiri mabadiliko ya muundo wa utumishi utakaotambua mabadiliko ya vyeo na majukumu ya kila siku.
Askari wa misitu wakionesha umahiri wao kwenye kutembea mwendo wa haraka na taratibu huku wakiwa na silaha wakati wakionesha kwa vitendo mafunzo ya kijeshi waliyopata katika kambi ya jeshi ya Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya kubadili utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeshwa katika mfumo wa jeshi usu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Costantine Kanyasu na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wajumbe wawili wa bodi, Wajumbe 19 wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya kijeshi yaliyofanyika katika kambi ya Mlele mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Costantine Kanyasu akikagua gwaride wakati wa kufunga mafunzo ya kijeshi kwa askari wa misitu 140 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yaliyofanyika katika kambi ya mafunzo ya Mlele mkoani Katavi.
Askari wa misitu wakionesha umahiri katika matumizi ya silaha wakati wakionesha kwa vitendo mafunzo ya kijeshi waliyopata katika kambi ya jeshi ya Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya kubadili utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeshwa katika mfumo wa jeshi usu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Costantine Kanyasu akitunuku vyeti kwa askari wa misitu waliohitimu mafunzo ya kijeshi katika kambi ya Mlele mkoani Katavi.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo (anayepiga makofi), viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wajumbe wa bodi na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira wakifurahia jambo baada ya askari wake kuonhyesha umahiri katika matumizi ya silaha wakati wakiomnyesha kwa vitendo jinsi wanavyoweza kupambana na adui kwa kutumia mbinu za kijeshi kama walivyofunzwa katika mafunzo ya kijeshi katika kambi ya Mlele mkoani Katavi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post