HAKIMU AAGIZA WAFUASI 18 WA CHADEMA WASAKWE


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuwasomea maelezo ya awali (PH) washtakiwa 31 wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema kutokana na washtakiwa wengine 18 kutofika mahakamani.

 Washitakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya mkusanyiko usio halali.

Wakili wa Serikali, Faraji Nguka alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Agustin Rwizile kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusoma maelezo ya awali (PH) lakini kuna washtakiwa ambao waliomba hati za kuwakamata na bado wanaendelea kuwatafuta.

"Tupo tayari kuendelea na hoja za awali licha ya wafuasi 18 kutokuwepo mahakamani, tulishaomba hati za kuwakamata bado tunaendelea kuwatafuta," amedai Faraji Nguka.

Wakili wa kujitegemea, Majura Magafu amedai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, huwezi kuendelea kama mshtakiwa hayupo mahakamani bila taarifa yoyote ya maandishi.

"Kesi inaruhusiwa kuendelea bila kuwakilishwa kama mshtakiwa atakuwa amewasiliana na wakili wake na kumpa taarifa tena kwa njia ya maandishi" amedai Wakili Magafu.

Wakili wa Utetezi, Alex Massaba amedai licha ya mahakama kutoa hati za kuwakamata washtakiwa, kumekuwa hakuna jitihada zozote za kuwatafuta.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Rwizile ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 17,mwaka huu kwa ajili ya kutolea uamuzi kama kesi hiyo iendelee na hoja za awali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post