WASHTAKIWA KESI YA KUSAFIRISHA DHAHABU MWANZA WAHUKUMIWA BAADA YA KUKIRI MAKOSA


Washtakiwa wanne kati ya 12 wa kesi ya jinai namba 1/2019 ya kusafirisha shehena ya dhahabu kilo 323.6 na fedha taslimu Sh305 milioni wamekiri makosa yao.

Washtakiwa hao ni wafanyabiashara Hassan Sadiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan..

Akitoa hukumu baada ya washtakiwa kukiri makosa yao leo Machi 27, 2019, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Rhodha Ngimilanga aliwahukumu washtakiwa kwenda jela kati ya miaka mitano hadi 15 au kulipa faini kati ya Sh5milioni hadi Sh100 milioni.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni wafanyabiashara Hassan Sadiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan waliokuwa wakitetewa na mawakili Emmanuel Safari na Michael Nasimile.

Pamoja na hukumu ya kifungo kwa muda tofauti na faini kulingana na makosa, Mahakama pia imeamuru kutaifishwa kwa kilo 319 za dhahabu, fedha taslimu Sh305 milioni, magari mawili, kilo sita za madini ya vito na mashine ya kupima ubora wa madini.

Katika hukumu yake, Hakimu Ngimilanga aliwatia hatiani washtakiwa katika mashtaka sita ambapo kwa shtaka la kwanza washtakiwa wote wanne wamehukumiwa faini Sh5 milioni au kifungo cha miaka 15 jela.

Katika shtaka la tatu Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa wa kwanza, Hassan Sadiq na kumhukumu kulipa faini Sh5 milioni au kwenda jela miaka 15.

Washtakiwa wote wanne pia wametiwa hatiani katika kosa la tano na kuhumiwa kulipa faini Sh600, 000 kila mmoja au kifungo jela miaka mitano.

Mahakama pia imewahukumu washtakiwa kulipa faini ya Sh600,000 kila mmoja au kifungo cha miaka mitano jela.

Mshtakiwa Hassan Sadiq pia ametiwa hatiani katika shtaka la nane na kuhukumiwa adhabu ya faini Sh5 milioni au kwenda gerezani miaka mitano.

Katika shtaka la tisa, washtakiwa wote kila mmoja amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh5 milioni.

Wakati wenzao wanne wakikiri makosa na kuhukumiwa, washtakiwa wengine wanane, wote wakiwa ni waliokuwa askari polisi akiwemo aliyekuwa mkuu wa operesheni mkoa wa Mwanza, Morice Okinda walikana mashataka na kurejeshwa rumande hadi Aprili 10, kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.

Wengine wanaoendelea na kesi ni E. 6948 D/CPL. Kasala, F. 1331 PL. Matete, G. 6885 D/C Alex, G. 5080 D/C Maingu, G. 7244 D/C Timothy, G. 1876 D/C Japhet na H. 4060 D/C David Kadama.

Washtakiwa hao walikamatwa kati ya Januari 4 na 5, 2019 wakisafirisha shehena ya dhahabu na fedha taslimu Sh305 milioni kinyume cha sheria.

Credit:Mwananchi


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527