UVCCM DAR WAZINDUA KAMPENI YA "DAR YA KIJANI" KURUDISHA MITAA NA MAJIMBO YALIYOCHUKULIWA NA UPINZANI


Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Dar es Salaam, umezindua kampeni ya ‘Dar es Salaam ya Kijani’ iliyolenga kurudisha mitaa na majimbo yanayoongozwa na vyama vya upinzani.

Pamoja na mambo mengine, kampeni hiyo inalenga kuweka mikakati kuanzia ngazi za jumuiya zote za mkoa huo, kuanza kujipanga kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Akizugumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Chuo Kikuu Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema kuwa kampeni hiyo itachochea ustawi zaidi wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuzidi kukita mizizi katika ngazi zote kuanzia mkoa hadi majimbo, wilaya hadi kata, na matawi hadi mitaa.

“Kampeni yetu ya Dar ya Kijani kuelekea serikali za mitaa 2019, ni kampeni kabambe kwa ajili ya kuirejeshea CCM mitaa iliyopotea katika uchaguzi uliopita ambayo kwayo itatusaidia kupata ushindi mkubwa kimkoa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 wa udiwani, ubunge na urais.

“Sote ni mashuhuda kwamba katika uchaguzi uliopita wa 2014 wa Serikali za Mitaa na ule Mkuu wa 2015 tulipoteza baadhi ya mitaa, kata na majimbo yaliyokuwa yakishikiliwa na CCM na sababu za kupoteza huko zinajulikana, sina haja ya kuzirejea sasa.

Hivyo sisi vijana wa CCM tunatambua kuwa ndiyo damu na roho ya chama chetu, na kwamba tunao wajibu wa asili wa kusafisha njia katika kutimiza malengo ya uwepo wa vyama vya siasa kikatiba ya kushika dola,” amesema Kilakala.

Aidha, amesema kampeni hiyo itashuka katika wilaya, kata na matawi yote jijini Dar es Salaam, ili kuhakikisha kila Kijana wa UVCCM anawajibika ipasavyo kuhakikisha falsafa ya Dar es Salaam ya kijani yaani Dar es Salaam ya CCM inaenea kwa wanachama na wananchi ili ikifika wakati wa uchaguzi tuvune wapiga kura wa kutosha.


Naye Katibu wa UVCCM mkoa wa Dar es salaam, Mwalimu Raymond Mwangwala aliwataka vijana nchini kuacha tabia ya kuwa wabeba pochi za watu, na kuomba nafasi za uongozi kuanzia ngazi za serikali za mitaa kwenye uchaguzi utakaofanyika mwaka huu 2019. 

Alisisitiza Dar es salaam lazima iwe mfano na vijana watoke na kuwa sehemu ya Historia ya Ujenzi wa Taifa la Tanzania chini ya Jemedari mkuu na Mzalendo, Rais John Joseph Magufuli.

Mwangwala alitoa rai kwa mikoa yote kuiga kampeni za namna hiyo zinazojenga Ari, hamasa na moyo wa kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Aliwakumbusha Vijana kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kuendesha kampeni mbalimbali lakini kujibia upotoshwaji unaofanywa na upinzani kila kunapokucha huku akiwataka vijana kufanya tafiti ili kusaidia kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527