SIMBA YAPOTEZA TENA UGENINI....YACHAPWA 2-0 NA JS SAOURASimba SC imeendeleza rekodi ya kupoteza mechi za ugenini katika Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya usiku huu kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji, JS Saoura Uwanja wa Agosti 20, 1955 mjini Bechar nchini Algeria. 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jean-Jacques Ndala Ngambo aliyepuliza kipyenga akisaidiwa na mshika kibendera Olivier Safari Kabene wote kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Soulaimane Amaldine wa Comoro, Saoura ilipata bao moja kila kipindi.

Alianza mshambuliaji Sid Ali Yahia Cherif dakika ya 18 kufunga kwa shuti kali akimalizia mpira uliorudi baada ya kuokolewa na Paul Bukaba kufuatia yeye mwenyewe kuunganisha kwa kichwa krosi ya Mohamed El Amine Tiboutine kutoka upande wa kulia.

Akafuatia Mohamed El Amine Hammia kufunga bao la pili kwa penalti dakika ya 51 baada ya Sid Ali Yahia Cherif kuangushwa na beki wa Simba SC, Paul Bukaba Bundala kwenye boksi.

Kwa matokeo hayo, Saoura inapanda kileleni mwa Kundi D ikifikisha point inane baada ya kucheza mechi tano, sasa ikifuatiwa na Al Ahly, AS Vita zenye pointi saba kila moja, wakati Simba SC sasa inashika katika Kundi D kwa pointi zake sita.

Mechi za mwisho Machi 16, Al Ahly na JS Saoura nchini Misri na Simba SC na AS Vita mjini Dar es Salaam zitaamua timu za kwendsa Robo Fainali kutoka Kundi D. 

Kikosi cha JS Saoura kilikuwa; Abderraouf Nateche, Nacereddine Khoualed, Ibrahim Bekakchi, Mohamed El Amine Barka, Mohamed El Amine Tiboutine, Ziri Hammar/ Thomas Ulimwengu dk79, Mohamed El Amine Hammia, Adel Bouchiba, Messala Merbah, Ibrahim Farhi na Sid Ali Yahia Chérif/ Moustapha Djallit dk88.

Simba SC; Aishi Manula, Serge Wawa, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba, Jonas Mkude/Muzamil Yassin dk84, James Kotei, Clatous Chama/Rashid Juma dk72, John Bocco, Meddie Kagere na Hassan Dilunga/Haruna Niyonzima dk46.
Via>Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post