SERIKALI YATISHIA KUUFUNGA MGODI WA NORTH MARA

Na Issa Mtuwa - Tarime 
Serikali imesema itaufunga mgodi wa North Mara ifikapo Machi 30, 2019 endapo mgodi huo utashindwa kuyadhibiti maji yenye sumu yanayo tiririka kutoka kwenye mabwawa ya kuhifadhia maji (topesumu) (Tailings Storage Facility -TSF). 
ya mgodi huo kuelekea kwenye makazi ya watu. 

Hayo yamesemwa leo machi 5, 2019 na Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko alipotembelea mgodini hapo kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea mabwawa wa topesumu (TSF) na kuzungumza na uongozi wa mgodi na baadae na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyamongo wilaya ya Tarime kuzungumzia hatima ya malipo ya fidia za wananchi waliohamishwa kupisha shuguli za mgodi. 

Biteko amesema serikali hairidhishwi na namna mgodi wa North Mara kwa jinsi wanavyo zingatia swala la utunzaji wa maji yenye sumu kwenye (TSF) zao. Amesema serikali inathamini sana maisha ya watu na mtu mmoja mmoja, na kwamba maisha ya mtu mmoja ni bora kuliko shuguli zote za mgodi. 

“ Naomba niseme ukweli, tena kutoka moyoni, sijaridhishwa na hili jambo la utiririshaji wa maji yenye sumu kuelekea kwenye makazi ya watu. Serikali hii ya awamu ya tano ya Dkt. John Pombe Magufuli inathamini sana maisha ya watu wake kuliko kitu chochote. Thamani yamaisha ya mtanzania mmoja ni bora kuliko kinachochibwa hapa. Nitoe rai kwa mgodi ifikapo Machi 30, mwaka huu, hili jambo liwe limekwisha, kinyume cha hapo, nitafunga mgodi mpaka pale mtakapo tekeleza jambo hili” alisema Biteko. 

Kwa upande wa uongozi wa mgodi umesema, utatekeleza agizo hilo na kwamba juhudi za kudhibiti topesumu kuelekea kwenye makazi ya watu limepewa kipaumbele na kwamba ndani ya muda huo litakuwa limekamilika. 

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko aliambatana na baadhi ya Maafisa wa Wizara hiyo akiwemo Kamishna wa Madini Mha. David Mlabwa na Afisa Madini mkoa wa Mara Mha. Nyaisara Mgaya, wengine ni kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa mara wakiongwa na mwenyekiti wake ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Mara bwana Adam Kigoma Malima. 

Ziara hiyo inafuatia vikao mbalimbali vya awali vilivyofanyika mwaka huu vikilenga masuala mbalimbali yanoyo husu mgodi huo likiwemo swala la udhibiti wa maji yenye sumu (topesumu) yanayo lalamikiwa na wananchi wanaoishi kuzunguka mgodi huo, kikao cha kwanza kilifanyika Januari 19, chini ya makatibu wakuu wa wizara saba ((Madini, Makamu wa Rais Mazingira (NEMC), Ardhi, TAMISEMI, Afya, Fedha na Maji)) ambapo serikali ilitoa miezi nane kutekeleza maagizo yaliyopewa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527