Serikali imesema kuwa itaendelea kuweka mazingira rafiki, kuwahamasisha na kuwavutia Wawekezaji watakaosaidia kuwapeleka watalii katika maeneo ya Kanda ya Ziwa ili kukuza Sekta ya Utalii Katika maeneo hayo.
Hatua hiyo inakuja baada ya kuyapandisha hadhi Mapori ya Akiba ya ya Burigi, Biharamulo, Kimisi,Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi ya Taifa.
Akizungumza kwenye mkutano uliohusisha Wizara Maliasili na Utalii na Wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta binafsi kwa kuwa sekta hiyo ni injini ya Utalii nchini.
Amesema kuwa mkutano huo una umuhimu mkubwa Katika maendeleo ya sekta hiyo kwa kuwa Serikali inapata nafasi ya kuwaelezea Wawekezaji fursa mbalimbali zinazopatika katika Ukanda huo pamoja na kusikia changamoto zao.
Amesema kufuatia kufanyika kwa mkutano huo Sekta Binafsi itakuwa na kila sababu ya kuwekeza katika Ukanda huo baada ya Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa Uwekezaji
Amesema Serikali imeendelea kuweka Miundombinu wezeshi ambayo imekuwa chachu ya kurahisisha watalii na wageni mbalimbali kutembelea maeneo ya hifadhi.
Mhe.Kanyasu ameyataja maeneo yaliyoboreshwa kuwa ni Barabara, Uwanja wa ndege wa Mwanza pamoja na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Chato ambao umefunguliwa.
Hata hivyo, Mhe.Kanyasu amesema kuwa licha ya kuwa Tanzania imekuwa ikifanya vizuri kwenye shughuli za Uhifadhi, lakini katika Uendelezaji Utalii bado jitihada za makusudi zinahitajika.
"Tuna vivutio vingi vya utalii lakini idadi ya watalii wanaotembelea vivutio hivyo hairidhishi, tunahitaji kuongeza juhudi katika kuwahamasisha watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea maeneo hayo" Amesisitiza
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye alikua mwenyeji wa mkutano huo, Prof.Adolf Mkenda amesema kupitia mkutano huo kutasaidia kuchagiza idadi ya watalii kuongezeka kwa kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana katika ukanda huo.
Amesema kufanyika kwa mkutano huo ni muendelezo wa kutawanya fursa za uwekezaji wa sekta ya utalii nchi nzima.
Akichangia hoja kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Watalii ( TATO)Wilbard Chamburo ameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutobadili mara kwa mara sera na mipango ya kukuza masuala ya Utalii kwa kuwa kuwa hali hiyo inayochangia kuwakatisha tamaa Wawekezaji.
Amesema Wawekezaji wanataka kuwekeza mahali ambako wana uhakika wa kupata faida itayowasaidia kujiendesha kibiashara pamoja na kulipa kodi stahiki za serikali.
Katika mkutano huo, Wakuu wa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhe.John Mongela walikua miongoni mwa Washiriki.