Timu ya Tanzania Prisons imeendelea kufanya vyema chini ya kocha wake mpya, Mohammed Rishard ‘Adolph’ baada ya jioni ya leo kuichapa mabao 2-0 JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Pongezi kwa wafungaji wa mabao hayo katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua Vedastus Mwihambi na Adam Adam.
Na kwa ushindi huo, Tanzania Prisons inafikisha pointi 38 baada ya kucheza mechi 30 na kujiinua kutoka nafasi ya 12 hadi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu inayoshirikisha timu 20.
Hali ni mbaya kwa JKT Tanzania iliyocheza mechi ya kwanza leo tangu imsimamishe kocha wake, Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ wiki iliyopita, kwani inabaki na pointi zake 36 baada ya kucheza mechi 31 na inateremka kwa nafasi mbili hadi ya 14.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Stand United wameibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex huko Kishapu mkoani Shinyanga.
Mabao ya Stand United yamefungwa na Datius Peter na Jacob Masawe, wakati bao pekee la Mwadui FC limefungwa na Salim Aiyee.
Stand United inafikisha pointi 36 baada ya ushindi huo katika mechi 31 na kujiinua hadi nafasi ya 11 kutoka ya 17, wakati Mwadui FC inateremkia nafasi ya 10 ikibaki na pointi zake 36 za mechi 31.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu unafuatia hivi sasa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam wenyeji, Azam FC dhidi ya Singida United.
Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tano zaidi, Lipuli FC wakiikaribisha Yanga SC Uwanja wa Samora mjini Iringa, Coastal Union wakiwa wenyeji wa Alliance FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Biashara United na African Lyon Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Mbeya City dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Chanzo - Binzubeiry