NHIF TANGA YAJIPANGA KUTOA ELIMU YA KUTOSHA KWA WANANCHI KUHUSU BIMA YA AFYA ILIYOBORESHWA


Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Tanga NHIF umejipanga kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na Bima ya afya iliyoboreshwa.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Mfuko huo Mkoani Tanga, Ally Mwakababu wakati akizungumza na Mtandao huu kuhusu walivyojipanga kuhakikisha wanaongeza wananchi na kuboresha huduma zao.

Alisema iwapo wananchi wataweza kupata uwelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kuwa na kinga ya matibabu kabla ya kuugua wataweza kuwakomboa wananchi wengi.

“Hakuna mtu au kiongozi ambaye atakuwa tayari kuongoza wananchi ambao ni goigoi wa maradhi hivyo Bima ya afya tumejipanga kuhakikisha kwanza tunaongeza idadi ya wanachama lakini kupitia wao tutaweza kuboresha huduma katika vituo vya afya”,alisema Mwakababu.

Hata hivyo Mwakababu alisema kuwa licha ya mkoa wa Tanga kuwa wa pili kwa uandikishaji wa bima ya afya ya jamii CHF lakini bado eneo hilo hawakuweza kufanya vizuri zaidi hivyo kwa mwaka huu wamejikita katika kuongeza uhamasishaji zaidi.

Alisema wamejipanga kufanya hamasa kuanzia ngazi ya mkoa hadi
vijiji kwa kushirikisha viongozi wa kiserikali na kisiasa kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi ndani ya Tanga anaona umuhimu wa kuwa na kadi ya Bima.

Vile vile akiongelea kadi ya Bima ya Toto afya Mwakababu alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2017/18 waliweka lengo la kuandikisha watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ,3000 badala yake waliandikisha 913.

Huku kwa walioko katika ngazi ya sekondari na vyuo ambao wanatumia huduma ya Toto afya kadi waliweza kuandikisha 1435 kati ya malengo waliyojiwekea ya kuandikisha wanachama 3000.

“Tatizo kubwa ni mwamko mdogo wa wananchi kuona umuhimu wa kuwa na bima ya afya wao wanasubiri mpaka ugonjwa uwe mkubwa na kushindwa gharama za matibabu lakini kumbe kama wangeweza kujiunga mapema wasiweza kupata huduma bora”,alisema Meneja huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527