NEC YAPULIZA KIPENGA UCHAGUZI JIMBO LA JOSHUA NASSARI...UCHAGUZI MEI 19


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru Mashariki ni Mei 19, 2019.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Machi 31, 2919 mkoani Morogoro amesema tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha sheria ya taifa ya uchaguzi aliitaarifu Tume kuwepo kwa nafasi wazi ya ubunge katika jimbo hilo.

"Nafasi ya jimbo la Arumeru ipo wazi na imetokana na aliyekuwa mbunge Joshua Samwel Nassari kupoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika," amesema Jaji Kaijage.

Amesema amevitaka vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya uchaguzi wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo.

Machi 14, 2019 Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alimuandikia barua Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage kumtaarifu jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi kutokana na kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo.

Mikutano hiyo ni ule wa 12 wa Septemba 4 hadi 14 mwaka 2018, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16 mwaka 2018 na mkutano wa 14 wa 29 Januari hadi Februari 9 mwaka 2019.

Na Lilian Lucas, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527