Sunday, March 17, 2019

JOSHUA NASSARI KUTINGA MAHAKAMANI KUFUKUZIA UBUNGE WAKE

  Malunde       Sunday, March 17, 2019

Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema atakwenda mahakamani kutafuta haki ya uwakilishi wa wananchi wa Arumeru baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kutangaza kwamba hana sifa za kuendelea na ubunge.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Machi 17, 2019 Nassari amesema mara ya mwisho alihudhuria mkutano wa Bunge wa Septemba lakini hakuhudhuria mkutano wa Novemba na Januari kwa sababu alikuwa anamuuguza mke wake huko Marekani.

"Nilifanya jitihada za kuwasiliana na Spika, nikamtumia ‘email’ (barua pepe) nikiwa Marekani kumjulisha hali ya mke wangu. Nasikitika kwa uamuzi alioufanya, nawapa pole wananchi wangu wa Arumeru, haki yao tutaitafuta kwenye vyombo vya sheria," amesema Nassari.

Akizungumza kwa huzuni, Nassari amesimulia jinsi alivyokuwa akimuuguza mke wake kutokana na matatizo aliyokuwa nayo na kusema alijaaliwa kupata mtoto wa kike Januari 27, siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge la Januari.

Amesema alikuwa njia panda kuamua kati ya kuhudhuria vikao vya Bunge au kukaa na mke wake ambaye alikuwa mgonjwa, ambapo amekiri kuwa hajutii uamuzi wake wa kusimamia kiapo chake cha ndoa kwa kuamua kumuuguza mke wake.

"Pamoja na huzuni ya kuvuliwa ubunge, bado nina furaha ya kupata mtoto, kwani kuwa mbunge hakuondoi majukumu mengine ya kifamilia. Spika alihudhuria harusi yangu mwaka 2014, alikuwa anajua sina mtoto na nilimjulisha juu ya matatizo ya mke wangu. Alitakiwa kujiridhisha kwa kuniita na kunihoji badala ya uamuzi alioufanya," ameongeza Nassari.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bunge iliyotolewa Machi 14 ilieleza kwamba Nassari alikosa sifa za kuwa mbunge kwa kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Septemba, Novemba na Januari.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post