SHIRIKA LA AGAPE LAENDESHA MAFUNZO KWA VIONGOZI WA DINI NA MILA IRAMBA

Shirika la Agape AIDS Control Programme (AACP) limeendesha mafunzo kwa viongozi wa dini na mila 25 kutoka Halmashauri ya Iramba katika mkoa wa Singida kuwahamasisha viongozi wa dini na mila kutumia majukwaa ya kiroho na kimila kuielimisha jamii kuachana na vitendo vya ukatili. 

Lengo la mafunzo hayo  yaliyofanyika leo ni  kuwaomba viongozi hao wa dini na mila kutumia nafasi walizonazo kuishauri serikali kufanyia marekebisho ya sheria ya ndoa namba 5 ya 1971 hasa vipengele vya 13 na 17 kwa kuweka umri wa kuoa au kuolewa kuwa angalau kuanzia miaka 18 kwa wasichana na wavulana.

Katika kufanya uchechemuzi huo juu ya kuishauri serikali kufanyia marekebisho Sheria ya ndoa, viongozi wa dini na mila wameombwa kutumia Mpango Kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto-MTAKUWWA.

Kupitia mpango huo serikali imeweka dhamira ya kutokomeza ndoa za utotoni kutoka kiwango cha sasa cha kitaifa cha 37% hadi kufikia 10% ifikapo mwaka 2022. 

Sheria hii imekuwa ikitumiwa kama uchochoro na baadhi ya wanajamii hasa wazazi wasiowatakia mema watoto wao wa kike na kuwafanya kuwa chombo cha kuiingizia kipato familia. 

Hivyo, endapo sheria ya ndoa itafanyiwa marekebisho na kuweka bayana umri wa kuoa au kuolewa kuwa ni miaka 18, hakika serikali na jamii kwa ujumla itatimiza adhima yake ya kutokomeza ndoa za utotoni.
Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola akiwasilisha mada kwa viongozi wa dini na mila katika Halmashauri ya Iramba Mji mpya wa Kiomboi, Mkoani Singida.
Viongozi wa dini na mila wakifuatilia mada ukumbini.
Meneja Miradi wa AgapeMustapha Isabuda akiwasilisha mada kwa viongozi wa dini na mila  kwa njia ya vitendo.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Iramba Samwel Singu  akitoa mada juu ya sheria zinazowalinda wanawake na watoto ikiwemo sheria ya ndoa na mapungufu yake.
Afisa Uchunguzi wa TAKUKURU Bwana Benjamini Syaka Halmashauri ya Iramba akiwasilisha mada juu ya madhara ya jinsi rushwa inavyochangia kushamiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mchungaji wa KKKT Mch. Peter Myampanda wa kanisa la Mgongo  Halmashauri ya Iramba Mkoani Singida akiuliza swali kwa Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Bi Jane Ng'ondi juu ya kwanini Sheria ya ndoa isifanyiwe marekebisho ili kusaidia kupunguza maambukizi ya VVU.

Viongozi wa dini na mila wakiwa katika picha ya pamoja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527