HATIMAYE MBOWE NA MATIKO WAACHIWA KWA DHAMANA...WAMEREJEA URAIANIMwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge, Esther Matiko wameachiwa kwa dhamana baada ya kushinda rufaa ya dhamana katika Mahakama Kuu Dar es salaam.

Mahakama Kuu imetengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwafutia dhamana ,ambapo wameruhusiwa kuwa nje kwa dhamana na kuripoti mahakamani mara moja kwa mwezi badala ya polisi kila wiki

Hukumu hiyo imetolewa leo Machi 7, 2019 na Jaji Sam Rumanyika.

Wakati Jaji Rumanyika akisoma hukumu hiyo ulinzi mahakamani hapo ulikuwa umeimarishwa kwa askari wengi waliotanda sehemu mbalimbali za Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

"Hii ni rufaa mojawapo sijawahi kuiona Katika kazi yangu ya Ujaji. Maofisa wa mahakama kama mahakimu wanapaswa kutumia utashi wao kuamua haki za watu kwa kuzingatia Haki maana ni hatari sana kumnyima dhamana mtu bila sababu za Msingi 

“Hakuna mahala popote warufani wamezuiwa kusafiri Lakini Wakati huo huo wanatakiwa kuripoti Polisi kila Juma. Hii maana yake wamenyimwa Uhuru wa kusafiri na haki ya kufanya kazi .

"Kuanzia sasa, naagiza Mbowe na Matiko waachiwe huru mara moja na watatakiwa kuripoti mahakamani mara moja kwa mwezi badala ya polisi kila wiki " Amesema Jaji Rumanyika wakati akisoma hukumu hiyo.

Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.

Wawili hao walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Kisutu kufuta dhamana yao ambapo rufani yao ilipangwa kwa Jaji Sam Rumanyika.

Hata hivyo, baada ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi ulidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu. 

Hata hivyo,March 1 mwaka huu, Mahakama ya Rufaa chini ya jopo la majaji watatu Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika na Mwanaisha Kwariko ilitupilia mbali pingamizi hilo la Serikali na kuamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post