CHADEMA WAMPIGIA SALUTI ZITTO KABWE


HATUA ya Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo kushawishi na hatimaye waliokuwa viongozi waandamizi wa CUF kujiunga na chama chake, imepongezwa. 

Akimkaribisha Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na timu yake aliyokwenda nayo Makao Makuu ya ACT-Wazalendo tarehe 18 Machi 2019, Zitto alisema hatua ya viongozi hao kujiunga na chama chake imepongezwa na vyama mbalimbali vya upinzani vikiongozwa na Chadema.

“Tunawashukuru Chadema kwa kutupongeza kwa hatua hii ya viongozi waandamizi wa CUF kuhamia ACT-Wazalendo. Nimefarijika kupata ujumbe wa pongezi kutoka kwa Mbowe (Freeman Mbowe-Mwenyekiti Chadema-Taifa), Dk. Mashinji (Dk. Vincent Mashinji-Katibu Mkuu Chadema), Mwalimu (Salum Mwalimu-Naibu Katibu Mkuu Zanzibar) na wengine.

“Niseme tu changamoto na mitihani ambayo vyama vya siasa hususani upinzani vinayopitia kwa sasa ndiyo inayotulazimisha tushirikiane kwa pamoja. Malaki ya wanachama wa CUF wanaohamia ACT-Wazalengo wana matumaini makubwa, tunapaswa kuyatekeleza,” alisema Zitto.

Zitto alisema, hatua ya Maalim Seif na timu yake kuhamia ACT-Wazalendo ni ya kuimarisha demokrasia Tanzania Bara na visiwani. “Na uimarishaji huu tutaufanya Bara na Visiwani.”

Akizungumza na wajumbe pia wanachama wa ACT-Wazalendo waliojumuika pamoja katika mapokezi ya Maalim Seif na timu yake, Zitto alisema lipo la kujifunza baada ya kiongozi huyo wa zamani wa CUF kujiunga na chama chake.

“Imetupa fundisho kwamba, ukiwa kiongozi uliye kwenye mioyo ya wananchi, hawawezi kukutupa. Tujenge uaminifu kwa wananchi wanaotupa dhamana,” amesema Zitto.
Via >>Mwanahalisionline

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post