LOWASSA AFUNGUKA KIAINA KILIMCHOTOA CHADEMA 'SITAKI WATU WANIWEKEE MANENO MDOMONI'


Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewaomba Watanzania waliompigia kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 kumuunga mkono, Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Lowassa aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi huo kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama washirika vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na CUF alipata kura milioni sita huku Dk John Magufuli wa CCM akipata milioni nane.

Hata hivyo, Lowassa ambaye alijiunga na Chadema Julai 28, 2015 akitokea CCM, Machi Mosi 2019 alitangaza kurudi CCM.

Leo Jumamosi, Machi 9, 2019 Lowassa amekwenda Monduli mkoani Arusha ambako anakabidhiwa kadi ya uanachama na amezungumza na mamia ya wanachama waliojitokeza kumpokea.

“Nimerudi nyumbani msiniulize nimerudi kufanya nini, nimerudi nyumbani,” amesema Lowassa ambaye amesindikizwa na mke wake, Regina na mwanaye Fred

Akiendelea kuzungumza amesema, “Kwenye uchaguzi nilipata kura zaidi ya milioni sita si haba, naomba wote walionipigia kura tumuunge mkono Rais John Magufuli.”

“Nampongeza Rais John Magufuli kwa ushawishi wake ambao umenifanya nimerudi nyumbani,” amesema.

Huku akishangiliwa, Lowassa amesema, “Kwa Chadema nawashukuru viongozi na wanachama sana, sitaki watu wengine waniwekee maneno mdomoni.”
Na Filbert Rweyemamu, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527