TUNDU LISSU AMTAKA SPIKA NA KATIBU WA BUNGE KUREJESHA MARA MOJA MSHAHARA WAKE


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amemtaka Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai kurejesha mara moja mshahara na stahiki zake za kibunge pasina masharti yoyote.


Lissu amesema amesitishiwa mshahara na posho za kibunge tangu Januari 2019 bila kuelezwa sababu zozote za hatua hiyo na kusema anakusudia kuchukua hatua za kisheria kufikisha suala hilo, Mahakama Kuu ya Tanzania kudai haki zake.

Mnadhimu huyo Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametoa malalamiko hayo jana Jumatano Machi 13, 2019 kupitia waraka uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukizungumzia jinsi anavyonyimwa stahiki zake za msingi akiwa mbunge.

Lissu amesema tangu Septemba 7, 2017 ameshindwa kuhudhuria shughuli za kibunge kutokana na kuwa nje ya nchi baada ya kushambuliwa na risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana kisha kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi.

Katika waraka huo, Lissu amezungumzia sheria na taratibu ambazo mbunge anaweza kukosa sifa ya kuwa mbunge ambazo yeye bado anazo ni pamoja na mtu kuhama chama, kuteuliwa kuwa makamu wa rais au kuchaguliwa kuwa rais.

“Ninautaka uongozi wa Bunge yaani Spika Ndugai na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai kurudisha mshahara wangu na posho za kibunge bila masharti yoyote,” amesema Lissu.

Amesema Bunge likiwa mhimili mkubwa wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali, linapaswa kuheshimu sheria, kusimamia haki na taratibu zake na kuzingatia misingi ya haki katika utendaji wa kazi zake.

“Ili kuhakikisha sheria za nchi yetu zinaheshimiwa na haki inatendeka, ninawaelekeza mawakili wangu nchini Tanzania kuanza mchakato wa kufungua mashauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania ili kudai Bunge la Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai lirejeshe stahili zangu zote zilizozuiwa na kulizuia lisiziingilie na kuziathiri kwa namna nyingine yoyote,” amesema Lissu.

SOMA ZAIDI HAPA
Chanzo - Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527