LIPUMBA APITISHWA KUGOMBEA UENYEKITI CUF NA WENGINE WAWILI


 Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) limewapitisha wanachama watatu wa chama hicho akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.

Akizungumza kwenye mkutano wa saba wa chama hicho leo Jumatano Machi 13, 2019 Profesa Lipumba amesema kwa sababu ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya uenyekiti hawezi kuwa mwenyekiti wa kikao hicho.

Amesema kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za chama hicho kikao kipendekeze mwenyekiti wa muda.

Aliwauliza wanachama kwa ujumla wao wanamtaka nani awe mwenyekiti wa muda wakajibu. ‘Milambo Yusuph Kamili’ hivyo akamtangaza kuwa ndiyo mwenyekiti wa muda wa kikao hicho.

Awali, Profesa Lipumba ametoa ufafanuzi wa uchaguzi utakavyofanyika kuwa wataanza na kumchagua mwenyekiti wa taifa, akifuatia makamu mwenyekiti Zanzibar na kumalizia na makamu mwenyekiti Tanzania Bara.

Pamoja na Profesa Lipumba wengine kwenye kinyang’anyiro hicho ni Diana Daudi Simba na Zuberi Mwinyi Hamisi. Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe 798.

Naye Mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya amesema kinachoendelea sasa hivi ni kuchagua wajumbe watakaoshiriki uchaguzi huo.

Kambaya amesema hali ya leo katika mkutano huo itakuwa nzuri tofauti na ilivyokuwa jana. Pia amesema kutakuwepo na ulinzi wa askari ambao watakuwa wamevaa nguo za kiraia ili kuhakikisha hali ya usalama inakuwapo.

Na  Kalunde Jamal na Hellen Hartley, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527