BOB WANGWE ASHINDA RUFAA YAKE KESI YA MAKOSA YA MTANDAO

Mahakama  Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam dhidi ya Bob Chacha Wangwe kulipa faini ya Sh. 5,000,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Akisoma hukumu ya rufaa dhidi ya hukumu hiyo jijini jana, Jaji Seif Mwishehe Kulita, alisema Bob Wangwe alihukumiwa kimakosa kwa kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani ikiwa ni pamoja na kutokuitwa mahakamani kwa mashahidi muhimu waliotajwa katika shauri hilo kutoka mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) kuthibitisha madai dhidi yake.

Akitaja mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kutoa hukumu katika kesi ya makosa ya mtandaoni, Jaji Kulita alisema ni lazima mtuhumiwa awe ametoa taarifa hiyo yeye mwenyewe, iwe imethibitishwa kuwa ni taarifa ya uongo na pia kama imelenga kuleta taharuki.

Rufaa hiyo namba 370 ya mwaka 2018 ilitokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya mshtakiwa huyo aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka ya kusambaza ujumbe uliodaiwa kwenda kinyume cha Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Bob Wangwe, mahakama hiyo ilimtia hatiani na kuamuru alipe faini ya Sh. 5,000,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya hukumu ya jana, Bob aliishukuru Mahakama Kuu kwa kutenda haki katika kesi hiyo na kuwashauri Watanzania kutokata tamaa na kuridhika pale wanapohisi kuwa wameonewa katika hukumu zinazotolewa na mahakama za chini dhidi yao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post