LUGOLA AWATAKA VIJANA KUTUNZA WAZEE WAO..HAKUNA ATAKAYESALIMIKA MAUAJI YA WAZEE

Waziri Mambo ya Ndani Kangi Lugola ametoa wito kwa vijana wote nchini kuachana na tabia ya mauaji ya vikongwe na Wazee Nchini na kutoa onyo kwamba hakuna muuaji hata mmoja atakaye salimika na kukwepa mkono wa sheria.

Amesema hayo jana jijini Dodoma katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi kilichowakutanisha wazee makamanda wa jeshi la polisi na maofisa Ustawi wa Jamii kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa kujadiliana kwa pamoja kuhusu mbinu mpya za kutokomeza mauaji hayo kwa kutumia Mkakati mpya wa miaka 5 wa Kutokomeza Mauji ya Wazee na Vikongwe Nchini.

Mkakati huo uliozinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Tanzania tarehe 29, January 2019 wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii Nchini uliofanyika Jijini Dodoma.

Aidha Waziri Lugola amewataka vijana kutambua kuwa kijana wa leo ni Mzee wa Kesho hivyo atambue kuwa machungu ya mauaji ya wazee wanayoyapata leo naye ayatarajie baadae kwa kuwa kila mtu atazeeka.

Kufuatia hali hiyo Waziri Lugola aliwataka Vijana kutunza wazee wao kwasasababu machozi ya wazee wanayolia kila siku kwa kwa kukosa matunzo ya watoto wao yanapelekea wazee wengi kuwa na macho mekundu yanayoplekea watu wenye imani potofu kuwapoteza maisha yao kwa imani za kishirikina.

Aliongea kuhusu Mkakati wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee Waziri Nchini Lugola alisema lengo la mkakati huu ni kuhakikisha tunashirikiana ili ifikapo mwaka 2023 mauaji ya wazee yawe yamekomeshwa kabisa.

”Hatutakua na sababu yoyote ya kueleza tukishindwa kutekeleza wajibu huu muhimu wa kulinda uhai wa kundi hili tete. Naomba muongeze kasi ili tufikie lengo hili, tena ikiwezekana mapema zaidi kwani tutapimwa kwalo 2023’’. Aliongeza Mhe. Lugola.

Alitoa wito kwa vyombo vya dola hasa Jeshi la polisi kuendelea kufuatilia kwa ukaribu sababu na vichocheo vya mauaji haya ikiwa ni pamoja na kuwabaini wahusika wanaopanga na kutekeleza mauaji haya ili wafikishwe kwenye vyombo vya Sheria, na pale inapothibika wahusika wachukuliwe hatua kali ili tukomesha kabisa vitendo hivi vya kikatili. 

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu aliwaambia wajumbe wa Mkutano kuwa mahuaji ya vikongwe yalianza tangu miaka ya 1960 na serikali imekuwa ikipambana nayo lakini yamekuwa yakiendelea.

Dkt. Jingu aliongeza kuwa jughudi za serikali kupitia Jeshi la Polisi zimefanikiwa kupunguza mauaji haya lakini hayajakwisha kwasababu bado kuna watu wengi wenye Imani potofu katika Jamii hivyo ni lazima mapambano dhidi yao yaendelee.

Alisema kuwa Mkakati wa Kutokomeza Mauaji dhidi ya Wazee unalenga kuwa na Taifa linaloazingatia haki na ustawi wa wazee kwa kupiga vita imani za kushirikina, ubaguzi, ukatili na mauaji.

Aidha Dkt. Jingu aliongeza kuwa tafiti zilizopo zinaonesha mauaji na ukatili dhidi ya Wazee yanachochewa na Imani za kishirikina pamoja na migogoro ya ardhi hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau imeandaa Mkakati wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee Nchini kwa lengo la kutokomeza kabisa mauaji haya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post