Katika hali ambayo haikutegemewa, Mkutano kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un umevunjika.
Mkutano wa siku mbili kati ya viongozi hao waliokutana nchini Vietnam umelazimika kuahirishwa baada ya kutofautiana katika masuala ya msingi, hivyo hawakufikia lengo la kutia saini nyaraka zozote.
Waandishi wa habari walishangazwa na taarifa ya kuahirishwa kwa chakula cha mchana kati ya viongozi hao ambacho walitarajia kushiriki kuchukua matukio.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba alitoka kwenye mkutano huo kwasababu ya masharti yasiyowezekana ya kiongozi hiyo ya kutaka nchi yake iondolewe vikwazo ilivyowekewa kwa uchochezi wa Marekani.
“Ndoto yetu na ndoto yao havikushabihiana. Wao walitaka kuondolewa vikwazo katika maeneo yote, na hatukuweza,” alisema Trump.
“Hatujakata tamaa, kuna uwezekano. Anataka kuachana na silaha za nyuklia, [Kim] anataka kufanya kwenye maeneo ambayo yana umuhimu kidogo kuliko tunavyotaka. Wakati mwingine inabidi kuondoka na wakati huo ulikuwa leo,” aliongeza.
Hata hivyo, Trump amemuelezea Kim kama kiongozi mzuri na kwamba anaamini wakati mwingine watafikia muafaka. Amesema ingawa mkutano huo haukuzaa matunda yaliyotarajiwa, kuna hatua ambazo zimepigwa kulinganisha na ilivyokuwa awali.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amewaambia waandishi wa habari kuwa katika makubaliano ya awali walibaini kuwa hakukuwa na kitu ambacho kingeifaidisha ipasavyo Marekani.
Amesema timu ya nchi hizo mbili itakutana tena kuendelea kujadiliana kwa mara nyingine ili wafikie muafaka.