TEHAMA YARAHISISHA MCHAKATO WA AJIRA SERIKALINI


Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi (aliyekaa mbele) akiongoza jopo la wajumbe wa usaili lililokuwa Dar es Salaam wakiendesha usaili kwa njia ya Video kwa mwombaji kazi wa nafasi ya Meneja wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko.
Muonekano wa uendeshaji wa usaili kwa njia ya Video. 
Wajumbe wa Jopo la Usaili wakiongozwa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Xavier Daudi (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Bw. Waziri Kindamba (wa pili kutoka Kushoto) wakijadiliana jambo kabla ya usaili wa mahojiano kwa njia ya video kuanza.
***

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imezidi kuboresha huduma zake kwa kuanza kuendesha usaili wa mahojiano kwa njia ya mtandao (Video Conference) baada ya usaili wa kwanza kufanyika wiki hii kwa baadhi ya nafasi za Watendaji Waandamizi ambapo mmoja wa wasailiwa alikuwa mkoani Mbeya na wajumbe wa jopo la usaili wakiwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Wajumbe wa jopo la Usaili huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Bw Waziri Kindamba amesema kuwa Sekretarieti ya Ajira ni miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizoamua kufanya mageuzi katika kuhakikisha inaboresha huduma zake kwa wadau ili kuweza kuwafikia popote pale walipo kwa kutumia teknolojia katika mawasiliano.

Amebainisha kuwa hatua waliyoichukua Sekretarieti ya Ajira ni jambo la kuigwa na taasisi nyingine, kwanza kwa kuwa wabunifu, pili kuokoa muda na gharama kwa wasailiwa kusafiri na mwisho kuonyesha uzalendo kwa kutambua na kuamua kutumia miundombinu ya TTCL kuendesha usaili wake kwa waombaji kazi walioko nje ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema kuwa taasisi yake imejipanga kuhakikisha inasogeza huduma karibu na wadau wake ikiwemo kurahisisha mchakato wa Ajira kwa lengo la kuongeza ufanisi.

“Sekretarieti ya Ajira imeshafanya maboresho mengi tangu tulipokabidhiwa jukumu hili la kuendesha mchakato wa ajira serikalini, awali tulianza kwa kwa waombaji kazi kutuma maombi yao kwa njia ya posta na badae tukabadilisha na kuanza kupokea maombi kwa njia ya mtandao, kwa sasa tumejikita zaidi katika matumizi ya TEHAMA, kwa kuanzisha mifumo mbalimbali ili kurahisisha utendaji wa kazi na kuongeza ufanisi” amesema Daudi.

Daudi amefafanua kuwa baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni pamoja na mfumo wa wa kuendesha usaili kwa njia ya mtandao (video conference), mfumo ya upokeaji wa maombi ya kazi (Recruitment portal), mfumo wa kupanga wasailiwa waliofaulu usaili (Placement Management Information System) na mfumo wa kutoa taarifa kwa waliopotelewa na vyeti mbalimbali vya kitaaluma (Loss report management system) wakishakamilisha taratibu.

Ameongeza kuwa nia ya Sekretarieti hiyo kuendelea kubuni mifumo inalenga kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa kufanya mchakato wa ajira kutoka siku 90 hadi siku 52 kwa ajira mpya na kwa wale wanaohifadhiwa katika kanzidata kutumia muda wa wiki moja kwa mwajiri kupata mtumishi anayemuhitaji.

 Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi na kupunguza malalamiko ya ucheleweshaji wa michakato ya ajira na kuondoa hisia za upendeleo kwa kuwa anayepata kazi ni yule mwenye sifa na vigezo stahili na si vinginevyo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527