SIMBA SC YAREJEA TATU BORA LIGI KUU KWA KISHINDO BAADA YA KUICHAPA MWADUI FC 3-0


Simba SC imerejea ndani ya tatu bora kwenye Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 usiku wa leo dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 36 sawa na Lipuli FC baada ya kucheza mechi 15, lakini inapanda nafasi ya tatu kwa wastani wake mzuri wa mabao kuliko timu ya Iringa ambayo pia imecheza mechi tisa zaidi.

Yanga SC inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 55 za mechi 22, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 48 za mechi 21. 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Alfred Vitalis wa Kilimanjaro aliyesaidiwa na washika vibendera, John Kanyenye wa Mbeya na Leonard Mkumbo wa Manyara hadi mapumziko tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 3-0. 

Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere alianza kuifungia Simba bao la kwanza dakika ya 21 kwa kichwa akimalizia krosi ya Mzambia, Clatous Chama aliyenzishiwa kona fupi na kiungo mwenzake, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

Kiungo Muzamil Yassin akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 25 kwa shuti kali baada ya pasi ya Nahodha John Raphael Bocco kufuatia krosi ya beki Zana Coulibally kutoka Burkina Faso.

Mshambuliaji na Nahodha John Raphael Bocco akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 29 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya Niyonzima.

Kipindi cha pili, Simba ilipata pigo baada ya kiungo wake Muzamil Yassin kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jonas Mkude.

Mechi iliyotangulia jioni ya leo, Coastal Union ililazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wageni wakitangulia kwa bao la William Patrick dakika ya 37 kabla ya wenyeji kusawazisha kupitia kwa Raizin Hafidh dakika ya 65.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Zana Coulibally, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba, Pascal Wawa, James Kotei, Muzamil Yassin/Jonas Mkude dk60, Haruna Niyonzima, John Bocco, Meddie Kagere/Adam Salamba dk78 na Clatous Chama/Emmanuel Okwi dk70.

Mwadui FC: Mussa Mbisa, Revocatus Richard, Emanuel Kichiba, Frank Magingi, Joram Mgeveke, Iddy Mobby, Wallace Kiango, Abdallah Seseme, Fabian Gwanse/Ibrahim Irakoze dk87, Ditram Nchimbi na Gerard Mdamu/Salimu Aiyee dk46.

Via>>Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post