Picha : SAVE THE CHILDREN YATAMBULISHA MRADI WA LISHE ENDELEVU DODOMA


Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Binilith Mahenge akizungumza wakati mradi wa Lishe endelevu ukitambulishwa Dodoma

Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto la Save the Children kwa kushirikiana na Delloite,Manoff na PANITA limetambulisha rasmi mradi wa lishe endelevu kwa viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma ili kuimarisha hali ya lishe kwa wanawake,vijana na watoto.

Uzinduzi huo umefanyika leo Februari 28,2019 katika ukumbi wa Morena Hoteli Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa mkoa wa Dodoma,Mheshimiwa Binilith Mahenge.

Mradi huo wa Lishe Endelevu unalenga kuimarisha hali ya lishe kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa, wajawazito na wanaonyonyesha, vijana wa rika la balehe na watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano ambao ni waathirika wakubwa wa lishe duni.

Mahenge alisema mradi wa Lishe Endelevu ni fursa kwa wananchi wa Dodoma hivyo kuwaomba watendaji wa serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau wanaotekeleza mradi huo ili wafanye kazi katika mazingira ya amani na utulivu kufikia malengo ya mradi.

“Malengo ya mradi huu kimsingi yanaimarisha afya na lishe ya jamii ambayo ni mtaji mkubwa katika kuimarisha nguvu kazi ya taifa haswa katika kipindi hiki cha mpito kuelekea uchumi wa kati”,alieleza mkuu huyo wa mkoa. 

“Tunawakaribisha sana wadau wetu wa Lishe Endelevu na tuwatakia heri na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa malengo ya mradi. Twendeni tukiwa tunakumbuka kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya Jamii, mkoa na Taifa kwa ujumla, viongozi na watendaji wa mradi huu tekelezeni majukumu yenu kama yalivyoainishwa kwenye malengo ya mradi”,alisema.

Katika hatua nyingine alisema Lishe duni haiathiri tu maendeleo ya mtoto lakini pia inaathiri ukuaji wake kimwili na kiakili kutoka kipindi cha ujauzito na hatimaye kuathiri mchango wake katika maendeleo ya taifa kwa kipindi chote cha uhai wake hivyo mradi huo utasaidia kuondokana na changamoto hizo.

Aidha aliwaomba wadau wa lishe mkoani Dodoma kuongeza jitihada kupunguza utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano ingawa  takwimu za hivi karibuni (TDHS 2015/16) zimebaini kuwa Udumavu umepungua kutoka asilimia 56.0 (2010) hadi asilimia 36.5 mkoani humo. 

“Hali ya lishe ya wanawake walio katika umri wa uzazi (miaka 15-49) nayo bado ni mbaya; sote tunajua, hali ya lishe ya mama ikiwa mbaya inaathiri hali ya mtoto toka tumboni pamoja na malezi na makuzi ya mtoto. Tafiti za hivi karibuni zimebaini kwamba, kati ya wanawake kumi, wastani wa wawili wana utapiamlo",aliongeza. 

Alibainisha kuwa lishe duni kwa wanawake wajawazito inachochea hatari ya kujifungua watoto njiti, waliodumaa au kuharibu mimba hivyo vifo vya wanawake wajawazito vitapungua sana endapo serikali kwa kushirikiana na wadau watakuwa na mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto mbalimbali zinazomkabili mama mjamzito, aliyejifungua na mtoto chini ya miaka mitano.

Kwa upande wake,Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Dodoma Benety Malima aliwaomba wadau wa lishe mkoani humo na serikali kushirikiana katika kutekeleza mradi huo ambao utasaidia kuimarisha hali ya lishe kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa, wajawazito na wanaonyonyesha, vijana wa rika la balehe na watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Malima alisema  mradi huo unatekelezwa katika mikoa minne ya Dodoma, Rukwa, Iringa na Morogoro kwa kipindi cha miaka minne Kwa miaka minne mradi utagharimu USD 19.7 Milioni ukifadhiliwa na Mfuko wa Watu wa Marekani ‘USAID’.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Binilith Mahenge akitoa hotuba wakati Shirika la Save the Children kwa kushirikiana na Delloite,Manoff na PANITA likitambulisha mradi wa lishe endelevu kwa viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Binilith Mahenge akitoa hotuba wakati mradi wa lishe endelevu ukitambulishwa kwa viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma.
Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Dodoma Benety Malima akiandika dondoo muhimu wakati Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Binilith Mahenge akitoa hotuba wakati mradi wa lishe endelevu ukitambulishwa kwa viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma.
Viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma wakiwa ukumbini.
Picha ya pamoja viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo mkoa wa Dodoma baada ya mradi mradi wa lishe endelevu kutambulisha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527