MWENYE NYUMBA ATUPWA JELA KWA UHARIBIFU KWENYE CHUMBA CHA MPANGAJI

Mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam Zamazam Mohamed amehukumiwa na Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, Dar es Salaam kwenda jela miezi sita au kulipa na faini ya Sh 600,000, baada ya kufanya uharibifu kwenye chumba cha mpangaji wake na kusababisha upotevu wa mali yenye thamani ya Sh 390,000.


Akisomewa hukumu hiyo na Hakimu wa mahakama hiyo, Mark Mochiwa, amesema mahakama hiyo imejiridhisha pasipo na shaka, kwamba Februari 28, mwaka jana, eneo la Mkwajuni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam mshitakiwa alivunja mlango wa chumba cha mlalamikaji Ovano Vitus.

Amesema katika uvunjaji wa mlango wa chumba hicho, ulisababisha upotevu wa simu pamoja na video, vyote vikiwa na thamani ya fedha hizo.

Shahidi namba moja wa mlalamikaji Issa Mohamed, alidai alipopigiwa simu na mlalamikaji na kufika eneo la tukio alikuta mlango umevunjwa na kwa muda wa siku mbili haujajengwa.

Amedai kuwa, hata walipokwenda serikali ya mtaa na kumtaka mshitakiwa afike kujielezea alikataa, baadaye walifika ofisi za kata na alipoitwa tena aligoma ndipo wakaamua kwenda kuchukua RB katika kituo cha polisi cha Oysterbay ambapo alikamatwa.

Lakini pia shahidi ambaye pia aliitwa na mshitakiwa alithibitisha kwamba mlango wa mlalamikiwa ulikuwa umevunjwa na wakati huo ulikuwa ukijengwa, kwa madai alimtaka mpangaji huyo aondoke na kumwachia chumba chake.

Wakati huohuo, watu wawili wamepandishwa kizimbani akiwemo dereva Hamidu Mussa (25) katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni kwa tuhuma za kuvunja na kuiba vitu vyenye thamani ya Sh 860,000.

Mussa wakati akisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Felister Massawe na Mwendesha Mashitaka konstebo wa polisi, Januari Kasekwa alidai kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 10, mwaka jana, eneo la Kinondoni Shamba Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alidai kwamba mshitakiwa alivunja nyumba ya malalamikaji Joseph Simba, na kuiba radio Sabufa, compyuta, video, CPU, kioo pamoja na maganda ya simu, vyote vikiwa na thamani hiyo.

Mshitakiwa alikana mashitaka hayo, kesi hiyo imeghairishwa hadi Februari 20 itakapotajwa tena. Dhamana ipo wazi ambapo alihitajika kuwa na wadhamini wawili watakaotimiza masharti ya dhamana na kusaini ahadi ya milioni mbili.

Wakati huohuo, Jackline Elisha, mkazi wa Oysterbay alisomewa mashitaka ya kuiba mkoba wa Tuilumba Tala, wenye gharama ya Sh 60,000.

Mwendesha mashitaka Kasekwa alidai mbele ya Hakimu Massawe kwamba mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 3, mwaka huu, eneo la KKKT Msasani wilaya ya Kinondoni.

Chanzo - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527