MWAKYEMBE AIFAGILIA NEMBO MAALUM YA AFCON U17 ILIYOZINDULIWA LEO

Nembo maalum ya mashindano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON U17) imezinduliwa leo Alhamisi February 14 jijini Dar es Salaam.

Hafla ya uzinduzi wa nembo hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa jijini chini ya Usimamizi wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Mwakyembe ameipongeza Nembo hiyo na kusema kuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania hasa vivutio vya utalii.


"Nembo hii imebeba vitu vikubwa vitatu katika nchi yetu na mashindano haya. Kwanza imebeba dhana ya utalii. Kivutio chetu kikubwa cha Tanzania Kimataifa ni mlima Kilimanjaro. Tunauona hapa.


Lakini pili imebeba dhana ya uhifadhi. Tumeambiwa kuna pembe ya tembo na ya kifaru. Ambao ni wanyama wetu tunaowahifadhi kwa nguvu zetu zote. Tatu, yote haya yanahusu michezo na ndio maana kuna mpira," alisema Dk Mwakyembe.


Mkurugenzi wa masoko wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Aaron Nyanda alisema kuwa nembo hiyo imechorwa kwa lengo la kuitangaza Tanzania.


"Tulianzisha mchakato kwa watu kubuni nembo ambayo tumeipata hii inayoonyesha vivutio vilivyopo hapa nchini. Na mshindi aliyeshinda atapata fursa ya kwenda nchini Peru ambako kutafanyika Fainali za Dunia kwa vijana wa umri huo iwapo tutafanikiwa kufuzu," alisema Nyanda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527