MSIBA WA RUGE WAKWAMISHA KESI YA HALIMA MDEE

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha usikilizaji wa kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, kufuatia shahidi wa upande wa mashitaka kushindwa kufika mahakamani. 

Wakili wa Serikali, Ashura Mzava ameiambia mahakama kuwa shahidi huyo ameshindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi wake, kutokana na msiba wa bosi wake, Ruge Mutahaba. 

Shahidi aliyeshindwa kufika Mahakamani, ni Abdul Mchembea, mfanyakazi wa Clouds Media Group Limited (CMG). Amefiwa na bosi wake – mkurugenzi wa matangazo -aliyefariki dunia juzi tarehe 26 Februari 2019, nchini Afrika Kusini.

Taarifa zinasema, Ruge alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya ini na figo.

Kesi hiyo ambayo iko mbele ya Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Hakimu Simba amesema, kutokana na dharura hiyo kesi imeahirishwa mapaka tarehe 21 Machi mwaka huu.

Mdee anadaiwa kutenda kosa hilo tarehe 3 Julai 2017 akiwa makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Mdee anatuhumiwa kutamka maneno kuwa “anaongea hovyo hovyo, anatakiwa afunge breki;” na kwamba kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527