CHADEMA WAMJIBU NDUGAI KAULI YAKE YA KUTAKA KUSITISHA MSHAHARA WA TUNDU LISSU



Tundu Lissu

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KAULI YA SPIKA WA BUNGE JOB NDUGAI KUTAKA KUSITISHA MSHAHARA WA MBUNGE TUNDU LISSU

Leo tarehe 07.02.2019 tumeisikia kauli nyingine tena ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa anasitisha mshahara na malipo yote ambayo Mhe.Tundu Lissu anastahili kulipwa kwa mujibu wa Katiba na sheria zetu.

Spika ametoa tangazo hilo siku chache tangu alipotoa matangazo mengine mawili kuwa anafikiria kumfuta Ubunge na alishamlipa fedha za matibabu kiasi cha shillingi milioni 250, jambo ambalo ilikuja kuthibitika Kuwa ni uongo na Spika alisema amenukuliwa kimakosa!

Spika wa Bunge ametoa kauli hizi katika kipindi ambacho anapambana kuonyesha kuwa Bunge analoliongoza sio 'Dhaifu' kama ambavyo alinukuliwa akisema CAG na ambaye aliitwa kwenye kamati ya Bunge ili akathibitishe kauli yake kuwa 'Bunge ni dhaifu' na tangu alipoenda mbele ya Kamati Spika hajawahi kuelezea UMMA kama kamati ililubaliana na hoja za CAG kuwa Bunge ni dhaifu ama laa!

Tunapenda kumkumbusha Spika wa Bunge kuwa 'taasisi' isiyofuata Sheria na Kanuni ambazo imejiwekea na badala yake ikafuata kauli na matamko ya mtu yaliyo kinyume na sheria na kanuni za taasisi katika kujiendesha ni taasisi dhaifu Sana.

Tunamkumbusha Spika wa Bunge kuwa wapo wabunge wengi kwenye historia ya Bunge letu ambao wamewahi na wengine wapo kwenye matibabu na haijawahi kutokea tukashuhudia kiwango kikubwa cha chuki dhidi yao kama ambavyo sasa tunashuhudia kwa Mhe.Lissu ambaye jaribio la mauaji lilishindikana kwa miujiza ya Mungu.

Tunamtaka Spika wa Bunge ajue kuwa wabunge kama Prof. Mwandosya, Dr. Mwakyembe, Job Ndugai na Sasa Tundu Lissu na Nimrod Mkono ni miongoni mwa wabunge ambao wamelazwa hospitalini kwa kipindi kirefu na katika historia ya Bunge hatujawahi Kuona kauli za chuki kama ambavyo zinatolewa dhidi ya Mhe.Lissu.

Chadema tunasikitishwa Sana na kauli hizi kwani ni uthibitisho wa wazi kuwa Bunge lilipokataa kulipia matibabu ya Lissu walikuwa wana nia Mbaya dhidi ya maisha yake na walipoona watanzania wameendelea kulipia matibabu yake imewaumiza !

Chadema tunamtaka Spika wa Bunge asimamie sheria na kanuni za Bunge na ajue kuwa wabunge wana haki ambazo zipo kwa mujibu wa Sheria na hawafanyi kazi zao kwa kutegemea fadhila.

Tunawaomba Wanachama wetu wamuombee Spika pamoja na wabunge ili waachane na 'roho za chuki' dhidi ya mbunge !ambaye Mungu alimuokoa baada ya kupigwa risasi 16 zilizoingia ndani ya mwili wake.

Tunapenda kumkumbusha Spika Ndugai kuwa haki huinua Taifa.

Imetolewa na;

John Mrema

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje

07 Februari, 2019

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527