MKUCHIKA AWAUMBUA WAKUU WA WILAYA WANAOSWEKA RUMANDE WATU KWA SAA 48

Waziri George Mkuchika.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika, amewaumbua baadhi ya wakuu wa Wilaya nchini wanaowaweka ndani watu kwa saa 48 wakati hakuna sheria inayowapa mamlaka hayo.

Mkuchika amewataka wakuu hao wa Wilaya kuacha kutumia mabavu kwenye utendaji wao wa kila siku kwa kuwa wakiendelea na tabia hiyo watakuwa wanahatarisha kazi yake ya uwaziri.

Akiwa bungeni wakati akichangia na kueleza kuwa wakuu wa wilaya na mikoa wanapaswa kutumia busara katika kuwaweka ndani raia, ambapo Waziri Mkuchika amesisitiza Wakuu wa Wilaya wasimponze.

“Msiniponze. Mimi nataka Rais Magufuli asinibadili hapa, mimi nataka Rais Magufuli aseme mzee endelea, tuache masuala ya umwamba, nawaomba huko mliko msiniharibie kazi yangu. Mimi ndiye mwenye cheo cha utawala bora, mimi ndiye Waziri mwenye dhamana ya utawala bora, ukiendesha mambo kinyume cha utawala bora unaniharibia kazi,” alisema Mkuchika.

Akielezea madaraka ya wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watu saa 24, lugha iliyotumika ni kwa usalama wake, maana yake mtu ameua mtu, na jamaa zake wamekasirika wanataka kumpiga yule aliyeua na hapo ndipo dhana ya kumweka huyo mtuhumiwa ndani saa 24 inatumika kwa usalama wake.

Alisema mkuu wa wilaya akishamweka mtu huyo ndani ya saa 24 na muda huo ukamalizika, ikifika asubuhi ni lazima apelekwa mahakamani.

“Nataka niseme mahali popote mkuu wa wilaya kumweka ndani mtu saa 48 ni makosa kwa sababu sheria inampa saa 24 na mkuu wa mkoa amepewa saa 48, na pia siyo lazima umuweke.” alisema Mkuchika.

Januari 29, mwaka huu Rais Magufuli akiwa kwenye hafla ya kuwaapisha majaji, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapya Ikulu jijini Dar es Salaam, aliwataka wakuu wa wilaya aliowateua kwenda kusimamia sheria, kutoitumia vibaya sheria ya kuwaweka watu polisi.

Chanzo:Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post