MKURUGENZI ANAYEDAIWA KUUA KANISANI AFUNGUKA "NIMEPAKAZIWA TU"


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Pius Luhende anayedaiwa kuhusika na mauaji ya Isaka Petro (28) amezungumza na Mwananchi akisema “nimepakaziwa tu.”

Luhende alitoa kauli hiyo baada ya mwandishi wetu kumtembelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida alikolazwa tangu Jumanne wiki hii baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.

Kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Ng’hungu Kuzenza, Luhende anasumbuliwa na pumu (asthma) na mapigo ya moyo.

Mkurugenzi huyo ni miongoni mwa watu saba wanaoshikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo yaliyotokea Jumamosi iliyopita katika Kanisa la Wasabato Kijiji cha Kazikazi mkoani humo.

Inaelezwa kuwa mauaji hayo yalitokea baada ya Luhende kuwafuata watuhumiwa wa kosa la kuharibu mali ya mlalamikaji Rose Andrew aliyedai kuharibiwa mali yake iliyopo ndani ya shamba la Tanganyika Packers linalomilikiwa na halmashauri hiyo.

Taarifa ya Polisi inasema kuwa Luhende alipoingia ndani ya kanisa hilo ilitokea vurugu na akaamua kutoka nje kabla ya askari wanyamapori waliokuwa na silaha kufyatua risasi kadhaa na moja ikampiga Isaka na kufariki dunia papo hapo.

Hata hivyo, waumini waliokuwepo katika kanisa hilo wakati mauaji hayo yakitokea walizungumza na Mwananchi na kupingana na polisi wakisema kuwa mkurugenzi huyo ndiye alimfyatulia risasi Isaka.

Luhende ambaye alikuwa akilindwa na askari kanzu wanne wodini alisema bado kifua kinambana mara kwa mara hasa nyakati za usiku.

“Hata hivyo, namshukuru Mungu kwa kunipigania naendelea vizuri kuliko nilipokuwa hospitali ya Manyoni,” alisema Luhende ambaye alikuwa amejilaza kitandani huku mikononi akiwa hajafungwa pingu.

Na Gasper Andrew, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post