AUAWA AKIAMUA UGOMVI WA WANANDOA WALIOKUWA WANAPIGANA NDANI KWAO

Picha haihusiani na habari hapa chini

Mkazi wa Lizaboni Manispa ya Songea mkoani Ruvuma, Mohammed Hamim, ameuawa kwa kupigwa na kipande cha bomba la chuma kichwani alipokuwa akiamulia ugomvi wa mume na mke ambao ni majirani zake. 

Akizungumza na Nipashe jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushy, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tatu usiku katika mtaa wa Pacha Nne, kata ya Lizaboni .

Kamanda Mushy alisema siku hiyo ya tukio hilo, Hamim alikuwa amekwenda nyumbani kwa Soud Mdoka baada ya kusikia kelele zilizokuwa zikiashiria kuomba msaada na baada ya kufika, aliwakuta Mdoka na mke wake, Paulina Mlenga (35) wakiwa wanapigana.

Alisema baada ya kuona hivyo, Hamim alianza kuwaamulia jambo ambalo lilisababisha apigwe na kipande cha bomba la chuma kichwani na kumsababishia kifo papo hapo.

Mushy alisema Mdoka baada ya kubaini kuwa amemfanyia kitendo kibaya jirani yake kwa kumpiga na kufa papo hapo, alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Kutokana na kitendo hicho, Kamanda Mushy alisema Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka Mdoka na akipatikana atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu mashtaka ya mauaji yanayomkabili.

Pia alisema mke wake, Paulina Mlenga, anashikiliwa na polisi katika jitihada za kumtafuta mume wake na mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea kwa uchunguzi.

Gideon Mwakanosya

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527