KILICHOENDELEA LEO MAHAKAMANI KATIKA KESI YA MBOWE NA VIGOGO WENGINE CHADEMA

Kesi namba 112/2018 inayowakabili baadhi ya viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na wabunge wengine saba wa chama hico, imeendelea leo, Alhamisi, Februari 14, kwa kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.


Kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ambaye aliteuliwa kuwa Jaji, ilitajwa leo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kevin Mhina, ambapo shauri la kesi hiyo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa na bado linasubiri rufaa ya kupinga dhamana iliyokatwa na upande wa mashtaka dhidi ya Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, ambayo itaanza kusikilizwa Februari 18, 2019 katika Mahakama ya Rufaa.


Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 28, 2019 kwa ajili ya kutajwa huku akieleza kuwa itapangiwa hakimu mara baada ya rufaa kusikilizwa.

Novemba 23, 2018 Jaji Mashauri alipokuwa hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya Kisutu alifuta dhamana kwa Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.

Baada ya uamuzi huo, washitakiwa hao wanaowakilishwa na wakili Peter Kibatala walikata rufaa mahakama kuu kupinga kufutiwa dhamana.

Hata hivyo, baada ya mahakama kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Upande wa Serikali ukiongozwa na mwanasheria, Paul Kadushi ulikata rufaa katika mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi uliotolewa na kuiomba mahakama kuacha kuendelea kusikiliza rufaa hiyo kwa sababu haina mamlaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post