SERIKALI YASIMAMISHA LESENI YA UCHAPISHAJI NA USAMBAZAJI WA GAZETI LA THE CITIZEN


Serikali imesimamisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la The Citizen kwa siku saba kuanzia leo Jumatano, Februari 27, 2019.


Uamuzi huo uliotolewa na Idara ya Habari (Maelezo) unatokana na madai ya gazeti hilo la Kiingereza kuandika habari iliyohusu maoni ya wataalamu walioelezea kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania na kuchapishwa Februari 23, 2019.

Barua ya Februari 27, 2019 ya kusimamishwa kwa The Citizen iliyosainiwa na msajili wa magazeti, Patrick Kipangula kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) inaeleza kuwa adhabu hiyo inahusu pia mtandao wa gazeti hilo.

“Katika habari hiyo kwa makusudi uliandika habari za uongo na upotoshaji kwa kuaminisha umma wa Watanzania na kwamba thamani ya Shilingi ya Tanzania imeporomoka ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita pasipo kufuata utaratibu wa kisheria na kanuni za fedha ambapo viwango vya fedha ya Tanzania hutolewa na Benki Kuu ya Tanzania,” inasema aya mmojawapo ya barua hiyo.

“Uamuzi wa kusimamisha kwa muda leseni hiyo unatokana na mwenendo na mtindo wa habari na makala ambao kwa kiasi kikubwa unakiuka misingi ya maadili ya taalamu ya habari kwa upotoshaji wa mara kwa mara wa taarifa zinazohusu Serikali na uchochezi bayana unaokiuka masharti ya leseni,” inasema aya nyingine katika hiyo iliyotumwa kwenda kwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL).

Katika barua hiyo, Serikali imeeleza kuwa licha ya gazeti la The Citizen kuomba radhi mara kwa mara bado limeendelea na uandishi ule ule wenye utata na ikalitaka lijirekebishe na kuzingatia misingi ya taalamu ya habari na sheria za nchi.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari amesema licha ya habari hiyo, The Citizen limewahi kuchapisha habari nyingine inayokiuka misingi na maadili ya uandishi wa habari Julai 22, 2018. 

Habari hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘US Senator Raises Alarm on Tanzania” ilimnukuu seneta wa Jimbo la New Jersey nchini Marekani, Bob Menendez alieleza kuhusu mwelekeo wa ukuaji wa demokrasia nchini Tanzania.

Kufungiwa kwa gazeti la The Citizen, ambalo ni gazeti dada la Mwananchi, kwa siku saba kunamaanisha kuwa litarejea tena sokoni Alhamisi ijayo ya Machi 7, mwaka huu.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu amesema wamepokea barua hiyo kwa mshtuko, lakini watafuata maelekezo ya Serikali.

“Tumepokea agizo hilo la Serikali kwa masikitiko, lakini kama kampuni daima tunaamini katika kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, hivyo tutatumikia adhabu hiyo kama tulivyoelekezwa,” alisema Machumu.

Chanzo - Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post