MWANAMUZIKI BOBI WINE ATANGAZA KUGOMBEA URAIS UGANDA KUMNG'OA MUSEVENI

Mwanamuziki Bobi Wine ambaye ni mbunge amesema atawania urais nchini Uganda katika uchaguzi mkuu ujao akidhamiria kumwondosha madarakani, Rais Yoweri Museveni.

Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, amekiambia kituo cha televisheni cha Marekani cha CNN kuwa amejiandaa kumkabili Rais Museveni.

“Tuna Waganda wengi waliojiandikisha kama wapiga kura wapya, na hii ndiyo njia pekee ya kumwondosha Museveni,” amesema Bob Wine ambaye yuko ziarani nchini Marekani.

Alipoulizwa kama ana uwezo wa kukabiliana na Rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu, mwanasiasa huyo anayewavutia vijana wengi alijibu: “ Sawa, jambo hili limekuwa likijitokeza mara kwa mara na watu wengi wamekuja kwangu wakitaka niwanie nafasi hii.

“Tumekuwa tukijadiliana na timu yangu na lazima niseme tumeamua (yeye na timu yake) kwa dhati kabisa kukabiliana na Rais Museveni katika uchaguzi ujao wa Rais.

Museveni alishinda katika uchaguzi uliofanyika 2016 na kulingana na matakwa ya katiba hakuruhusiwa kuwania tena madaraka kutokana na umri wake lakini marekebisho yaliyofanyika baadaye yalimwondolea kizingiti hicho.

Pia, Bunge la nchi hiyo lilipitisha marekebisho ya sheria kwa kurefusha muhula wa Rais kuwa madarakani kutoka miaka mitano hadi kufikia saba. Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527