YANGA WAIBUTUA MWADUI FC 3-1...AJIBU NOMAAYanga SC imeendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 3-1 Mwadui FC ya Shinyanga katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam jioni ya leo.


Ushindi huo umetokana na mabao ya viungo wazawa Ibrahim Ajibu Migomba na Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ pamoja na mshambuliaji mkongwe kutoka Burundi, Amisi Joselyn Tambwe.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 53 katika mechi ya 19, sasa ikiongoza Ligi Kuu kwa pointi 13 zaidi ya Azam FC inayofuatia katika nafasi ya pili ambayo imecheza mechi 17, wakati mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 33 za mechi 14.

Bao pekee la Mwadui FC inayobaki na pointi zake 24 za mechi 22 katika nafasi ya 11 lilifungwa na Salim Aiyee mwishoni mwa mchezo huo. 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Fikiri Yussuf wa Morogoro, aliyesaidiwa na washika vibendera Abdallah Rashid wa Pwani na Abdallah Uhako wa Arusha hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Akicheza kwa mara ya kwanza kama Nahodha wa timu, wadhifa aliopewa na kocha Mkongo, Mwinyi Zahera baada ya kuvuliwa beki Kelvin Patrick Yondan, Ajibu aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 12 kwa shuti la mbali mno, kwenye nusu yao ndani ya duara la katikati ya Uwanja.

Lakini Ajibu akampelekea mikononi shuti la mkwaju wa penalti kipa Arnold Massawe dakika ya 18, adhabu iliyotolewa baada ya Tambwe kuangushwa kwenye boksi.

Ajibu akafuta makosa yake kwa kumtilia krosi nzuri Tambwe kutoka upande wa kushoto na Mrundi huyo ambaye walianza kucheza naye tangu Simba SC akaifungia Yanga bao la pili kwa kichwa dakika ya 39.

Kipindi cha pili Yanga SC walirudi vizuri na kuendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa Mwadui FC, timu kutoka wilayani Kishapu mkoani Shinyanga na kwa mara nyingine Ajibu akaseti bao, safari hiyo akimpasia Feisal Salum kufunga bao la tatu dakika ya 57.

Yanga ikapata pigo baada ya beki wake wa kulia, Paulo Godfrey ‘Boxer’ kushindwa kuendelela na mchezo dakika ya 77 bada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na mkongwe Juma Abdul na Salim aiyee akaifungia Mwadui FC bao la kufutia machozi dakika ya 81.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Klaus Kindoki, Paulo Godfrey/Juma Abdul dk77, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Said Juma ‘Makapu’ dk82, Pius Buswita, Amissi Tambwe, Haruna Moshi/Andrew Vincent ‘Dante’ dk64 na Ibrahim Ajibu.

Mwadui FC; Arnold Massawe, Revocatus Richard, Emmanuel Kichiba, Frank Magingi, Joram Mgeveke, Iddi Mobby, Jean-Marie Girukwishaka/Wallace Kiango dk67, Ibrahim Irakoze, Salim Aiyee, Ditram Nchimbi na Ottu Joseph Samuel.

Via>Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post