WAZIRI WA KILIMO: IFIKAPO JUNI 2019 WAKULIMA WOTE WATAKUWA WAMESAJILIWA NA KUWA NA VITAMBULISHO


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo; Tunduru-Ruvuma
Wizara ya Kilimo imeanza kuandikisha wakulima nchini kwa lengo la kuwatambua ili kuwarahisishia huduma mbalimbali zikiwemo uhitaji wa pembejeo za kilimo.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo wakati akizungumza na Wenyeviti na makatibu wa Vyama vya Msingi kwenye kikao kazi kilichofanyika leo tarehe 6 Januari 2019 katika Ukumbi wa Claster Mjini Tunduru katika Mkoa wa Ruvuma.

Akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani Tunduma Waziri huyo amesema kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa taarifa zinazohusu uandikishwaji wa wakulima kuwa una lengo baya, hivyo amewataka wakulima hao kutosikiliza propaganda hizo zisizo na tija kwani utambuzi wa wakulima ni jambo la kawaida kufanya utambuzi.

Alisema kuwa kuandikisha kwa wakulima ni njia pekee ya kuwa na takwimu sahihi kwa kutambua idadi ya wakulima, vijiji na Kata wanazolima ikiwa ni pamoja na kutambua ukubwa wa mashamba yao kwani kufanya hivyo serikali itakuwa na urahisi wa kuwahudumia wakulima hao.

Katika hatua nyingine Mhe Hasunga amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe Juma Homera kwa kusimamia vyema sakata la korosho kwa kusikiliza kesi 11 huku zikifikishwa mahakamani kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

“Nakupongeza sana Mhe Homera kwa usimamizi madhubuti katika kudhibiti kangomba nilipata taarifa kuwa Kg 17,679 za korosho mmezikamata pamoja na zingine Kg 2,779.2 jambo hilo ni zuri endeleeni kusimamia vyema majukumu ya serikali ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM yam waka 2015-2020” Alikaririwa Mhe Hasunga

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe Juma Homera aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuanza kuwalipa wasafirishaji wa korosho kutoka maghala ya vyama vya msingi, kuwalipa gharama za uendeshaji kwa vyama vya masingi, kuwalipa watunza maghala na magunia sambamba na kuondoa mzigo kwa wakati kutokana na ghala kuezuliwa na upepo lililokuwa na jumla ya Tani 536.

Pamoja na pongezi hizo pia Homera amezitaja changamoto mbalimbali katika Oparesheni korosho kuwa ni pamoja na kuchelewa kwa malipo ya wananchi waliofanyiwa uhakiki, utaratibu wa upatikanaji wa miche ya korosho kwa msimu wa mwaka 2018/2019, na mkanganyiko wa upatikanaji wa mapato ya Halmashauri 3% ya bei ya korosho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post