Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamejipanga kumkabili kwa hoja Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kwa madai kuwa amekuwa kinara wa upotoshaji pamoja na kuwa mstari wa mbele kupinga mamlaka ya Spika Job Ndugai kufanya kazi zake.
Wabunge hao wa CCM ambao walikutana kwenye kikao chao mjini Dodoma jana, katika azimio la pamoja walisema watahakikisha wanapambana na Zitto kwa kujibu hoja zake na viongozi wengine wa Upinzani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kutoka kwenye kikao cha wabunge wa CCM jana mjini hapa, Mbunge wa Mbinga, Sixtus Mapunda alisema wameshangazwa na hatua za Zitto kwenda mahakamani kumzuia Spika kutekeleza majukumu yake.
Mapunda ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake wa CCM, alisema katika hali ya kushangaza na iliyo kinyume cha sheria, Zitto ameshirikiana na baadhi ya wanasheria kuzuia mamlaka ya Spika kutekeleza wajibu wake.
Jambo lingine ambalo limeonekana kuwa kero kwa wabunge wa CCM ni Mbunge huyo wa Kigoma Mjini kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) na kutuma nakala kwa Maspika wa Mabunge yote ya Afrika kwa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) pamoja na Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali wa Jumuiya ya Madola.
“Hatua ya Zitto kukimbilia Mahakamani kupinga Mamlaka ya Spika au kuandika barua kwa mabunge ya nchi nyingine kupinga uamuzi wa Spika au kujadili mamlaka yake kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni dharau kubwa kwa mamlaka ya Spika na Muhimili wa Bunge kwa ujumla.
Mapunda alisema kuwa kanuni ya 5(4) na (5) ya kanuni za Bunge, imeweka utaratibu kuwa mbunge kama Mbunge hakuridhishwa na uamzi wa Spika, anaweza kupinga uamuzi huo na atawasilisha sababu za kutoridhishwa kwake kwa Katibu wa Bunge na malalamiko hayo yatafanyiwa kazi na Kamati ya Kanuni za Bunge na baadaye Bunge litajulishwa kuhusu uamuzi utakaotolewa.
Naye Mbunge wa Mtera, Livingistone Lusinde ‘Kibajaji’, alisema Zitto amepoteza mwelekeo na anatakiwa kujitafakari ili arudishe heshima yake ya kisiasa badala ya kupambana na siasa za upotoshaji.
Lusinde alimtaka Zitto Kabwe kuacha kutumia siasa kama zilizokuwa zikifanywa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha DP, marehemu Mchungaji Christopher Mtikila za kushinda mahakamani kufungua kesi.
Alisema Zitto akiendelea kufanya siasa ambazo anaendelea nazo atashitakiwa na mke wa Mtikila.
“Zitto sasa hivi anachukua ‘style’ za Mzee Mtikila za kushinda Mahakamani badala ya kushinda kutafuta hoja na watu wake wa Kigoma.
“Yaani yupo ACT Wazalendo lakini akili anazotumia ni za hayati Mtikila, nadhani mke wa Mtikila kama kungekuwa na sheria ya kusimamia stahiki za mumewe ana uwezo wa kumshtaki Zitto ili aweze kumlipa fidia kwa kutumia jina la mumewe yaani Zitto Mtikila,” alisema.
Kuhusu kauli ya Zitto, Lusinde alisema kazi ya bunge si ya kubeza, iwe mbaya au nzuri ndiyo kazi ya Bunge.
“Mimi namuona kama vile siku hizi ametoka kwenye reli kwa sababu hata ukimsikiliza vizuri mimi nadhani ana tatizo kubwa sana.
“Unawezaje kusema sheria hii ikienda bungeni itapita kwa sababu wabunge wa CCM wote ni makasuku. Zitto anapaswa kujitafakari upya kwa sababu anakoelekea anaenda shimoni kabisa,” alisema Lusinde.