VITA YA UBUNGE YAANZA MAPEMA IRINGA, CCM WATAKA,MSIGWA AKOMAA


Vita ya kuwania Jimbo la Iringa Mjini imeanza mapema baada ya mwenyekiti mpya wa CCM mkoani humo, Dk Abel Nyamahanga kuahidi kulirejesha mikononi mwa chama hicho.

Hata hivyo, mbunge wa jimbo hilo, Mchungaji Peter Msigwa, amemjibu akisema hayumbishwi na kauli hiyo na kwamba CCM haiwezi kulichukua kwa kuwa Chadema ina wafuasi wengi.

Akizungumza juzi na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM baada ya kutangazwa mshindi, Dk Nyamahanga aliahidi kuwa atahakikisha jimbo hilo linarudi mikononi mwa CCM kwa njia yoyote akianza na kutatua changamoto za wananchi.

“Nashukuru kuchaguliwa kuwa mwenyekiti, ndoto yangu ni kuhakikisha navunja makundi ya baadhi ya wanachama na kuhakikisha tunaungana kuchukua jimbo kwa masilahi ya wananchi wanaokiamini chama kilichopo madarakani ambacho ni CCM,” alisema.

Mwenyekiti huyo alikuwa akirejea maagizo ya Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa aliyehoji kwa nini jimbo hilo liko chini ya chama cha upinzani na kuagiza katika uchaguzi wa 2020 lirudishwe CCM.

“Tunahitaji kufanya uchunguzi kwa nini jimbo lipo upinzani. 2020 ni muhimu likarudi CCM tu, nataka kujua je, ni wapigakura ndiyo tatizo au wana CCM wenyewe tunashindwa kusimamisha mgombea tunayemtaka?” alihoji Pinda.

Akizungumza na Mwananchi jana, Msigwa ambaye alishinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na 2015, alisema haoni kama CCM ina ubavu wa kulichukua jimbo hilo. Msigwa ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, alisema katika mkoa huo wafuasi wa Chadema ni wengi zaidi na haoni kama chama chake kitapokwa jimbo katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuwataka wanachama wake kuendelea kujenga imani kwa chama na viongozi mkoani humo.

“Tunajipanga vizuri kukabiliana na hali yoyote, hatutaki tupate mgombea mwepesi na tutawashinda kwa nguvu sana,” alisema.


Na Berdina Majinge na Cledo Michael mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post