TAKUKURU YAZIANIKA IDARA ZINAZOONGOZA KWA RUSHWA SHINYANGA

Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa  Shinyanga Francis Luena akizungumza na waandishi wa habari leo.


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga imetoa taarifa ya utendajikazi wake kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba 2018,katika kuchunguza,kuelimisha umma na kufanya utafiti,kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na.11 ya mwaka 2007. 


Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Januari 21,2019 Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Francis Luena alisema kwa kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba hadi mwezi Desemba 2018 wamepokea taarifa 90 ambapo idara ya polisi(10), elimu(12), mahakama(11), serikali za mitaa(10), ardhi(10), afya(7) na huduma za kifedha(7) zikitajwa kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa.  

TAKUKURU pia imetembelea miradi 9 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.424 na kubaini baadhi ya miradi kuwa na dosari. 

“Miradi yenye dosari ni pamoja na mradi wa machinjio na banda la kuanikia ngozi wilaya ya Kishapu ambao thamani yake ni shilingi milioni 12, fedha zinazochunguzwa ni shilingi milioni 4.3, pamoja na mradi ujenzi wa kituo cha mabasi baada ya kuufuatilia iligundulika shilingi milioni moja matumizi yake yalikuwa hayaeleweki,” alisema Luena. 

Luena alisema kesi zinazoendelea mahakamani ni 19 na kwamba taasisi hiyo imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa watumishi mbalimbali, kufanya uchunguzi wa vitendo vya rushwa na kwafikisha mahakamani wahusika. 

Alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano pindi wanapoona viashiria vya rushwa na kuwakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili na kufuata sheria na kanuni za utumuishi wa umma.

Na Malaki Philipo – Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527