SIMBA YAPEWA KICHAPO CHA MBWA KOKO...YASHINDILIWA 5 - 0, AS VITA NOMA SANA


Simba  SC imepoteza mechi ya kwanza Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 5-0 na wenyeji, AS Vita Uwanja wa Martyrs de la Pentecote zamani Kamanyola, uliopo eneo la Lingwala mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 

Kipigo hicho kinakuja baada ya Simba SC kuanza vyema mchezo wake wa kwanza ikishinda 3-0 dhidi ya JS Saoura ya Algeria Jumamosi ya wiki iliyopita mjini Dar es Salaam na kuwapa matumaini Watanzania kwamba inafanya vizuri.

Sasa Kundi D linapangika kama lilivyotarajiwa, Al Ahly wakiongoza kwa pointi zao nne, wakifuatiwa AS Vita pointi tatu sawa na Simba huku JS Saoura ikishika mkia kwa pointi yake moja. 

Mshambuliaji Jean-Marc Makusu Mundele ndiye aliyeanza kuwianua mashabiki wa AS Vita baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 14 akimalizia pasi ya Glody Ngonda Muzinga.

Beki Botuli Padou Bompunga aliyekuwa anacheaa badala ya Dharles Kalonji leo ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu, akaifungia AS Vita bao la pili dakika ya 19 akimalizia kona ya Ngonda. 

Kiungo Fabrice Luamba Ngoma akaifungia AS Vita bao la tatu kwa penalti dakika ya 45 na ushei akimtungua kipa namba wa Tanzania, Aishi Salum Manula kufuatia beki Muivory Coast wa Simba SC, Serge Wawa Pascal kumuangusha mchezaji huyo kwenye boksi.

Kocha wa Simba SC, Mbelgiji Patrick Aussems na wachezaji wake walimfuata refa, Mahamadou Keita na wasaidizi wake, Seydou Tiama, Sidiki Sidibe pamoja na mwamuzi wa akiba, Abdoulaye Sissoko wote kutoka Mali kuwalalamikia kwa uchezeshaji wao baada ya kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, Keita alikuwa mkali na kuwafukuza Aussems na wachezaji wake huku akionekana kama kuwatishia kuwaadhibu, nao wakaepusha shari kwa kuondoka zao kwenda kujipanga kwa kipindi cha pili.

Aussems alikianza kipindi cha pili kwa mabadiliko katika safu ya kiungo, akimtoa Muzamil Yassin na kumuingiza Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kabla ya baadaye kumtoa Mzambia, Clatous Chama na kumuingiza mzawa, Hassan Dilunga.
Lakini mabadiliko hayo hayakuwa na msaada kwa Simba SC, kwani jahazi lake lilizidi kuzama ikipachikwa mabao mawili zaidi na kupata cha 5-0.

Beki Makwekwe Kupa alifunga bao la nne kwa kichwa dakika ya 71 akimalizia kona nzuri iliyochongwa na Tuisila Kisinda, kabla ya Makusu kuwachambua mabeki wa Simba na kipa waop, Manula kuifungia Vita bao la tano dakika ya 74 kufuatia pasi nzuri ya Kazadi Kasengu.

Baada ya mchezo Aussems aliwafuata tena marefa, ingawa safari hiyo alionekana kama kuwashukuru na kuwapa ‘maneno ya busara’.

Kikosi cha Simba SC kinageuza kesho kurejea Dar es Salaam kucheza michuano ya SportPesa Super Cup kabla ya kusafiri kwenda Misri kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kumenyana na wenyeji, Al Ahly Februari 2.

Kikosi cha AS Vita leo kilikuwa; Nelson Lukong, Yannick Bangala/Makwekwe Kupa dk46, Nelson Munganga, Glody Ngonda, Botuli Padou Bompunga, Djuma Shabani, Ernest Sita, Fabrice Ngoma, Jean-Marc Makusu, Kazadi Kasengu na Tuisila Kisinda/ Ducapel Moloko dk78.

Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei, Muzamil Yassin/Haruna Niyonzima dk46, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Clatous Chama/Hassan Dilunga dk61.

Via binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post