JESHI la Polisi wilayani Serengeti mkoani Mara imepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanywa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).
Maandamano hayo yalikuwa yafanyike leo Jumatano Januari 9, 2019 ili kumpongeza mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya kwa jitihada zake za kuwatetea wastaafu kwenye suala la kikokotoo cha asilimia 25.
Barua ya kuzuia maandamano hayo imeandikwa na mkuu wa polisi wa wilaya hiyo, Mathew Mgema akisema suala la kusitisha kikokotoo cha asilimia 25 lilifanywa na Rais John Magufuli wakati alipozungumza na watumishi Desemba 28, 2018 na wala si Bulaya.
Polisi wamesema badala ya kufanya maandamano, wameshauri anaweza kuwasiliana na wananchi wake wa Bunda Mjini na kupanga namna ya kumpongeza Bulaya kwani ndio eneo lake la uwakilishi lakini si kufanya maandamano.
Mkuu huyo wa Polisi amesema hawatasita kuchukua hatua pale ambapo kuna ukiukwaji na dalili za uvunjifu wa amani.