VIGOGO NIDA WASOMEWA HATI MPYA YA MASHTAKA 100

Vigogo sita wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) akiwamo Mkurugenzi Mkuu wa zamani, Dickson Maimu, wamefikishwa mahakamani na kusomewa hati mpya ya mashtaka 100 yakiwamo 22 ya kughushi, nyaraka za kumdanganya mwajiri 43, kujipatia fedha mawili, matumizi mabaya moja na kutakatisha fedha na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh. bilioni 1.175.

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine ni Aveline Mombuli, Astery Ndege, George Ntaliwa, Xavery Silverius maarufu kama Sliverius Kayombo na Sabina Nyoni.

Walisomewa mashtaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali, Simon Wankyo na Leonard Swai. Wankyo alidai kuwa kesi hiyo namba 07/2019 ina mashtaka 100 dhidi ya washtakiwa hao.

Alidai mshtakiwa wa kwanza, wa tatu, wanne na watano wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama la kwanza na la 85.

Alidai kuwa Maimu, Ndege na Ntalima wanakabiliwa na mashtaka 22 ya kughushi nyaraka malipo kutoka Nida.

Upande huo wa Jamhuri ulidai Maimu, Ndege na Ntalima wanakabiliwa na mashtaka 43 ya kuandaa nyaraka za uongo za malipo ya kumdanganya mwajiri wao.

Swai naye alidai Maimu, Ndege, Ntalima na Kayombo, wanakabiliwa na mashtaka 25 ya kutakatisha fedha haramu.

Aliendelea kudai katika mashtaka matano mshtakiwa Maimu, Ndege, Ntalima, Kayombo, Mombuli na Nyoni kwa nyakati tofauti waliisababishia Nida hasara ya Sh. 1,175,785,600 walishindwa kutimiza majukumu yao na kupitia nyadhifa walizokuwa nazo waliisababishia hasara hiyo.

Katika shtaka la 95, ilidaiwa kuwa kati ya Novemba 7, 2011, makao makuu ya Nida ofisi zilizopo Kinondoni, Maimu akiwa mtumishi wa umma kama Mkurugenzi Mkuu na Nyoni akiwa kama Mkurugenzi wa Sheria walitumia madaraka yao vibaya na kusababisha Shule ya Sheria na Kampuni ya M-S Law Partner kujipatia faida ya Sh. 899,935,494.

Ilidaiwa Juni 5, 2013 katika Benki ya CRDB tawi la Lumumba, Ilala jijini Dar es Salaam Kayombo kuwa alijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh. 45,515,961, huku akijua ni mazalia ya kughushi na utakatishaji fedha haramu.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Swai alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na aliomba mahakama kupanga tarehe ya kuwasomewa washtakiwa maelezo ya mashahidi.

Pia, alidai wameshawasilisha taarifa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa kuhusu kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu alisema washtakiwa watasomewa maelezo ya mashahidi Februari 12, mwaka huu na wapelekwe mahabusu.

Alisema mshtakiwa wa pili, Mombuli na Nyoni, wanakabiliwa na mashtaka ya kuwasilisha nyaraka za kumdanganya mwajiri na matumizi mabaya ya madaraka wawasilishe upya maombi ya dhamana Mahakama Kuu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post