MAUAJI YA WATOTO YATUA BUNGENI..LUGOLA ASEMA NI USHIRIKINA

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amesema imebainika kuwa mauaji ya watoto mkoani Njombe ni ya imani za kishirikina.

Lugola ametoa kauli hiyo leo Jumatano Januari 30, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na mbunge wa Mufindi Kusini (CCM), Mendrad Kigola.

Mbunge huyo amehoji ni mkakati gani umewekwa na Serikali katika kukomesha mauaji ya watoto katika mkoa wa Njombe ili kurudisha amani mkoani humo.

Akijibu swali hilo, Waziri Lugola amesema tangu juzi Januari 28, 2019 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni yupo mkoani Njombe ambako anafanya vikao vya ndani na kamati za ulinzi ili kutafuta chanzo.

"Tumeshapata orodha ya majina ya wahusika na tumebaini sababu kubwa ni imani za kishirikina, lakini nawaonya wote wanaohusika kuwa wasitingishe kibiriti katika serikali ya Rais John Magufuli, watashughulikiwa," amesema Lugola.

Waziri amesema Serikali iko macho na itaendelea kuwa macho katika kuwalinda watu wake na vyombo vya ulinzi havitalala.

Na Habel Chidawali,Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527