MBOWE NI MGONJWA ASHINDWA KUFIKA MAHAKAMANI ..ZITTO KABWE AFUNGUKA


Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amekitaka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kutoa taarifa juu ya hali ya afya ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye ameshindwa kuwasili Mahakamani leo kwa sababu ni mgonjwa.

Zitto Kabwe ambaye ni moja ya viongozi wa Chama Cha ACT- Wazalendo ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake twitter na kudai kuwa taarifa za kiongozi huyo wa upinzani ni muhimu kwao.

Zitto ameandika, "Mwenyekiti Freeman mbowe leo hajatokea mahakamani, tumesikia ni mgonjwa, poleni sana na tupole wana demokrasia wote nchini, ni muhimu CHADEMA mjulishe umma hali ya Kiongozi wa Upinzani nchini maana tupo nyakati mbaya sana, tusidharau lolote lile".



@ChademaMedia Mwenyekiti @freemanmbowetz leo hajatokea mahakamani. Tumesikia ni mgonjwa. Poleni sana na tupole wana Demokrasia wote nchini. Ni muhimu CHADEMA mjulishe Umma hali ya Kiongozi wa Upinzani nchini maana tupo nyakati mbaya sana Hivi sasa. Tusidharau lolote lile
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, leo ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu zilizoelezwa kuwa ni mgonjwa.

Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, imeelezwa hayo leo, Alhamisi Januari 17, 2019 na wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita.

Mwita ameeleza hayo, mbele ya hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

“Mheshimiwa Hakimu, washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako, isipokuwa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hii, ambaye ni mgonjwa na leo ameshindwa kuletwa mahakamani hapa kusikiliza shauri hili," amedai Mwita na kuongeza.

“Kwa taarifa tulizopewa na wenzetu wa Magereza ni kwamba mshtakiwa Mbowe ni mgonjwa na leo ameshindwa kuletwa mahakamani hapa, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" amedai Mwita.

Wakili Mwita alidai kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri maamuzi kutoka Mahakama ya Rufani.

Baada ya kueleza haya, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi, Januari 31, mwaka huu. Upande wa utetezi leo uliwakilishwa na wakili Hekima Mwasipu.

Mbowe na Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Ester Matiko, wanaendelea kusota rumande kutokana na kufutiwa dhamana.

Mbowe na Matiko, walifutiwa dhamana, Novemba 23, 2018 na hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri baada ya kukiuka masharti ya dhamana.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 112/ 2018 ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Wengine ni Katibu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16 mwaka huu maeneo ya Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527