RAIS MAGUFULI AFUNGUKA KUHUSU WAKUU WA WILAYA NA MIKOA KUWEKA NDANI WATU

Rais John Magufuli amewaasa wakuu wa wilaya kutotumia vibaya sheria na mamlaka walizopewa ikiwamo za kuweka watu ndani na kuwatoa wakidai wamejifunza bila kupelekwa mahakamani.


Magufuli ameyasema hayo leo wakati wa kuwaapisha majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani.

Amesema siyo haki na viongozi wengi wamezungumza kuhusu suala hilo na yeye anarudia kwa sababu kama mkuu wa wilaya ana mamlaka hayo na mkuu wa mkoa akiamua kuweka watu ndani itakuwa ni vurugu, huku akibainisha kuwa mambo mengine yanahitaji kutolewa maelekezo tu.

“Kuelekeza kunaweza kuwa na matokeo chanya wakati mwingine kuliko hata kuweka watu ndani,” amesema.

Magufuli Magufuli amesema ameamua kumtoa katika uongozi aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho na kumhamishia katika kitengo cha wadudu kwa sababu yeye ni mtaalamu wa eneo hilo.

Amesema yaliyokuwa yakitokea wilaya ya Mwanga ya kuwaweka watendaji wa Serikali ndani akiwamo katibu tawala, mkurugenzi kila mmoja alikuwa akiyaona huku vurugu zote zilikuwa zikianzia kwa kiongozi huyo.

“Hata katika mazungumzo yake amekuwa akisema yeye ni mtaalamu pekee wa wadudu Tanzania hakuna kama yeye hivyo nikaamua kumpeleka huko huenda atafanya vizuri...” amesema Magufuli.


Na Aurea Simtowe, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527